Gavana Kahiga awachemkia waliosema ‘Ndindi Tosha’
NA MERCY MWENDE
GAVANA wa Nyeri Mutahi Kahiga ametishia kwamba migawanyiko inayoshuhudiwa katika eneo la Mlima Kenya itawaponza wakazi na wenyeji.
Kauli yake inajiri siku chache baada ya baadhi ya viongozi wa Murang’a kumuidhinisha Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro awe mgombea mwenza wa Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2027 na kisha awanie urais mwaka 2023.
Sasa gavana Kahiga akijibu kauli iliyotolewa na Seneta wa Murang’a Joe Nyutu, amekosoa vikali uidhinishaji huo uliofanywa kwa msingi wa ukuruba kati ya seneta huyo na mbunge huyo wa muhula wa pili.
Kwa upande wake, Bw Kahiga ametaka amani idumu na kwamba Naibu Rais Rigathi Gachagua ndiye atawapamba viongozi chipukizi katika eneo hilo.
“Yawezekana kwamba hatupendani lakini tuna wajibu wa kumuunga mkono Naibu Rais anapojizatiti kulitumikia taifa lakini pia akihakikisha nasi tunamegewa kipande cha keki ikizingatiwa kwamba siasa zetu ni za ushindani. Tukitofautiana wenyewe kwa wenyewe, wengine watakuwa na fursa kubwa dhidi yetu na hata tukapoteza nafasi ya naibu rais,” akasema Bw Kahiga.
Alisema uidhinishaji huo ulikuwa wa mapema mno na usiofaa.
“Hatuwezi tukatoshanisha nafasi ya Naibu Rais na kiti cha ubunge. Naibu Rais ni msaidizi wa Rais ambaye anaiongoza Kenya nzima lakini Bw Nyoro ni mbunge na mwenyekiti wa bejeti, nafasi za kawaida mno bungeni,” akasema.
Kwa sababu ya nafasi yake, Bw Kahiga anasisitiza Bw Gachagua ndiye kigogo wa eneo la Mlima Kenya mwenye wajibu wa kuwaandaa viongozi wanaoinukia kuepusha pengo kama lile lililoshuhudiwa wakati Rais wa Nne Uhuru Kenyatta alistaafu rasmi Septemba 13, 2022.
“Kwa sasa Ndindi Nyoro na Kimani Ichungwah ambaye ndiye Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, ni vigogo wa kesho lakini kwa sasa wakubali kupewa mwelekeo ili ifikapo 2032, wawe wameiva,” akasema.
Mapema wiki hii, seneta Nyuto kwenye mkutano wa kimkakati na viongozi wengine wa Murang’a, alimtaka Rais William Ruto kumteua kiongozi kijana wa Murang’a, ambaye ni Bw Nyoro akidai kwamba Bw Gachagua “alipotea njia, anawakosea viongozi heshima, hata waliochaguliwa.”
Naye mbunge wa Gatanga Edward Muriu alisema ni sharti Murang’a kupewa heshima kwa sababu kwa mujibu wa historia ya jamii ya Agikuyu hapo ndipo makao rasmi ya chimbuko lao.
“Wanawake wa Murang’a hata nao hujifungua watoto na Bw Nyoro ametosha kuwa naibu wa Ruto na kukwea kuwa kiongozi,” Bw Muriu akasema.