Ni wakati wa Taifa Stars baada ya mbwembwe za Mandonga ‘Mtu Kazi’
Na MWANGI MUIRURI
BAADA ya Tanzania kuburudisha vya kutosha kupitia visanga vya mwanabondia wao Karim Madonga ‘Mtu Kazi’ ambapo vichapo mfululizo vilimtuliza, macho yote yanaelelezwa kwa timu yao ya soka ya Taifa Stars itakaposhuka dimbani kukomoana na Morocco katika dimba la Taifa Bingwa Afrika (Afcon).
Tanzania likiwa ndilo taifa mwakilishi wa Afrika Mashariki katika dimba hilo, litakuwa limebeba matumaini na fahari ya kanda nzima.
Shabiki sugu wa Taifa Stars katika Kaunti ya Murang’a Bw Martin Kahiro anasema kwamba leo Jumanne ni kisa cha “amkeni tukashuhudie ‘Daudi’ Tanzania akizamisha ‘Goliathi’ Morocco”.
Kahiro ana matumaini kwamba TZ itafanya kweli.
“Mtanange huo utakuwa mgumu kwa Tanzania lakini vijana wa Afrika Mashariki wanaweza kupata ushindi wa aina yoyote ile,” akasema Kahiro.
Kipute hicho kilichong’oa nanga nchini Cote d’Ivoire mnamo Januari 13 kitaendelea hadi Februari 11, 2024.
Tanzania imepangwa katika ‘Kundi F’ pamoja na Morocco, DR Congo na Zambia na iko chini ya ukufunzi wa Adel Amrouche kutoka Algeria ambaye analenga kufikisha taifa hilo hadi hatua ya fainali na hatimaye kuinua kombe hilo.
Taifa Stars ambayo duniani imeorodheshwa katika nafasi ya 121 kwa umaahiri wa kandanda imeshiriki dimba hilo kwa mara mbili sasa (1990 na 2019) na ambapo katika hali hizo zote iling’olewa katika awamu ya makundi, matokeo bora zaidi yakiwa ni sare ya goli moja kwa moja huku ikilimwa katika hali michuano mingine 10. Hivyo hii ni mara ya tatu kwa TZ.
Taifa la Morocco ambalo limeorodheshwa kama la 13 kwa ubora wa viwango vya kandanda, limeshiriki dimba hilo kwa mara 18 ikiwa ni 1972, 1976, 1978, 1980, 1986, 1988, 1992, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2008, 2012, 2013, 2017, 2019, 2021 na sasa.
Timu hiyo ya Morocco ikinolewa na kocha Walid Regragui, iliweka rekodi katika Kombe la Dunia la mwaka 2022 nchini Qatar, ilitinga awamu ya nusu-fainali na kuweka rekodi kwa mataifa ya Afrika na Uarabuni.
Kwa sasa, Morocco ni miongoni mwa mataifa ambayo yanapigiwa upatu mkubwa wa kutwaa taji hilo la Afcon 2023 lakini Tanzania ikiwa hapo kuzuia balaa kwa Afrika Mashariki.
Tanzania ina kikosi imara, magolikipa wakiwa ni Kwesi Kawawa, Beno Kakolanya na Aishi Manula. Walinzi ni Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Nickson Kibabage, Lusajo Mwaikenda, Adam Kasa, Zion Chebe Nditi, Mark John na Miano Danilo.
Katikati mwa uwanja watategemea Yusuf Kagoma, Mzamiru Yassin, Sospeter Bajana, Adolf Bitegeko, Roberto Yohana, Edwin Balua, Said Hamis, na Tarryn Allarakhia.
Kutikisa nyavu wameaminiwa Kibu Dennis, Abdul Suleiman, Ladaki Chasambi, na Simon Msuva na Mbwana Samatta.
Kwa upande wa Morocco kikosi ni manyani El Mehdi Benabid, Yassine Bounou na Munir El Kajoui huku walinzi wakiwa ni Yunis Abdelhamid, Abdelkabir Abqar, Nayef Aguerd, Yahya Attiat-Allah, Mohamed Chibi, Achraf Hakimi, Noussair Mazraoui, Chadi Riad, na Romain Saiss.
Viungo wa kati ni Selim Amallah, Sofyan Amrabat, Oussama El Azzouzi, Bilal El Khannouss, Azzedine Ounahi na Amir Richardson huku wauaji wakiwa ni Amine Adli, Sofiane Boufal, Ayoub El Kaabi, Youssef En-Nesyri, Abdessamad Ezzalzouli, Amine Harit, Ismael Saibari, Tarik Tissoudali, na Hakim Ziyech.
Timu nyingine ndani ya kipute hicho ni wenyeji Cote d’Ivoire, Nigeria, Equatorial Guinea, na Guinea-Bissau katika ‘Kundi A’ huku ‘Kundi B’ likijumuisha Misri, Ghana, Cape Verde na Msumbiji.
Katika ‘Kundi C’ kuna Senegal, Cameroon, Guinea na Gambia huku ‘Kundi D’ likiwaleta pamoja Algeria, Burkina Faso, Mauritania na Angola. Mwisho, kuna ‘Kundi E’ likiwa na Tunisia, Mali, Afrika Kusini, na Namibia.