Sababu zilizofanya Lizzie Wanyoike kukimbilia maisha ya ndoa
NA MWANGI MUIRURI
KATIKA simulizi ya kusisimua kuhusu maisha yake ya ujana, marehemu Lizzie Wanyoike lau angeishi muda kidogo tu zaidi, angekuhadithia kuhusu kisa cha mwaka 1972 wanaume wawili walipokimbizana kwa magari wakimpigania.
Mwanamume mmoja kati yao alikuwa amemzidi Lizzie kwa umri na zaidi ya miaka 10 huku mwingine akiwa wa rika lake.
“Nilikuwa mwanafunzi katika Taasisi ya Kenyatta ambayo leo hii inafahamika kama Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU). Nilikuwa nimeingia kwa uhusiano na mwanamume huyo mkubwa kiumri lakini pia kijana wa rika langu alikuwa ananiwinda. Kipindi hicho niseme tu kwamba nilikuwa kwa mtanziko, nikitafakari nimchukue nani na nimteme yupi,” akasema Lizzie katika kitabu cha historia yake ambacho alikuwa anakielekeza kwa hatua za mwisho mwisho kukichapisha.
Bi Wanyoike anaelezea kwamba huyo mwanamume wa pesa nyingi alikuwa anamiliki gari aina ya Mercedes Benz.
“Alikuwa mwingi wa adabu na heshima,” akasimulia.
Alikuwa amemuambia kwamba “kwa muda nimekuwa nikikufuatilia na nimeamua kukupenda wewe tu uwe unaishi kwangu nikikuona kama maua na hatimaye unizalie watoto wa sura ya kupendeza kama hii yako iliyo na macho ya shaba”.
Lizzie alisema kisanga kilijitokeza Ijumaa moja ambapo mwanamume huyo alijitokeza chuoni mwendo wa saa kumi na nusu kumchota ampeleke jijini Nairobi kwa miadi ya usiku kucha.
“Huyu mzee alikuwa ni milionea lakini kijana naye alikuwa akionyesha nia ya kuwa na bidii na afanikiwe maishani. Uamuzi wangu ulikuwa kati ya kuamini ushahidi au nifuatane na matumaini… Nikaanguka kwa ushahidi wa milionea badala ya imani ya milionea mtarajiwa,” akasema.
Lizzie alisema kwamba aliingia katika gari la mwanamume huyo na wakaanza safari ya kuelekea jijini.
“Lakini kwa lango kuu nikaona gari aina ya Mini Morris la kijana aliyekuwa ananiwinda… Nusura moyo unisimame nilipoona akijaribu kutufungia njia. Hapo ndipo nilishuhudia niking’ang’aniwa kwa hatari ya mbio za magari,” akasimulia.
Alisema kwamba kilichojiri ni mfukuzano wa magari hadi jijini Nairobi.
“Mwanamume niliyekuwa naye aling’ang’ana kumhepa kijana lakini wote wawili wakibakia ‘bampa kwa bampa’. Walikimbizana hadi kwa chochoro za jijini, tukaelekea hadi Kilimani, tukashuka tena hadi katikati mwa jiji kabla ya mzee kuamua sasa liwe liwalo, lazima angempoteza kijana huyo. Aliamua kuingia katika barabara kuu ya Nairobi kuelekea Mombasa,” akasema.
Bi Wanyoike alisema kwamba alidhani siku ya kifo ilikuwa imewadia wakati mwanamume alisema angekimbia naye hadi Mombasa na “kijana akitaka kufuata afuate tu”.
Mbio ziliishia Mlolongo gari la kijana lilipoisha mafuta na “kupitia vijichochoro, tukarejea jijini Nairobi eneo la Westlands”.
Lizzie alisema kwamba nusura apoteze wote wawili siku hiyo lakini busara ya mzee ikasimama na akachukulia tukio hilo kama ushahidi wa mshikaji kuwa ‘mali safi’.
“Kijana hakujitokeza maishani mwangu tena nami tokea siku hiyo nikaamua kuingia kwa maisha ya ndoa na mzee huyo ambaye ndiye mnanifahamu naye katika jina langu la Wanyoike,” akamalizia kisa.
Marehemu Lizzie atazikwa Gatanga mnamo Januari 23, 2024.