Habari za Kitaifa

Mkopo mwingine: Wakenya kukamuliwa ushuru zaidi kulipa malimbikizi ya madeni

January 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

SHIRIKA la Fedha Duniani (IMF), Alhamisi liliidhinisha Kenya kupewa mkopo mpya wa Sh150 bilioni.

Kinaya ni kuwa, hili ni licha ya utawala wa Kenya Kwanza wake Rais Ruto, kusisitiza kuwa unafanya kila uwezalo kupunguza deni ambalo Kenya inadaiwa na mataifa ya nje na taasisi za kifedha za kimataifa.

Kwenye utaratibu wa utoaji wa fedha hizo, shirika hilo kwanza litatoa Sh99.6 bilioni kwa Kenya.

Hatua hiyo inafuatia mkutano uliofanyika Jumatano baina ya maafisa wa Wizara ya Fedha na shirika hilo, kutathmini mkataba na makubaliano baina ya Kenya na shirika hilo.

Mkutano huo uliamua kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo mara moja.

“Ustawi wa Kenya bado umebaki thabiti licha ya changamoto nyingi kiuchumi kutoka ndani na nje ya nchi. Makubaliano yaliyopo ni sisi kuendelea kuunga mkono taasisi zilizopo kulirejesha taifa kwenye uthabiti wa kiuchumi,” likasema shirika hilo.

Kutokana na mkopo huo, kiwango cha fedha ambazo shirika hilo limetoa kwa Kenya kama mikopo zilifikia Sh701.8 bilioni.

Kuidhinishwa kwa mkopo huo kunafuatia ziara ya maafisa kadhaa wa IMF jijini Nairobi kati ya Oktoba 30 na Novemba 15 mwaka uliopita, wakiongozwa na Bw Haimanot Teferra.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya kiuchumi, ijapokuwa serikali imekuwa ikisema inaweka mikakati ya kupunguza ukopaji kutoka nje, Kenya bado ina safari ndefu kujitoa kwenye shimo la madeni mengi.

“Itatuchukua miaka kadhaa kurejea kwemye uthabiti kamil wa kiuchumi. Pia, hilo litategemea mikakati itakayowekwa na serikali,” asema mwanauchumi Tony Watima.

 Kufikia sasa, deni la Kenya linakisiwa kuwa karibu Sh11 trilioni.