Makala

Kinda anayekuza mihogo

January 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SAMMY WAWERU

OPARESHENI kukabiliana na upungufu wa chakula na baa la njaa hasa katika maeneo kame, ni suala linalohitaji ubunifu katika kilimo.

Kando na kukumbatia teknolojia na mifumo ya kisasa kuongeza kiwango cha mazao, wanazaraa wanahimizwa kukuza mimea inayostahimili makali ya jua na kiangazi.

Hamasa hiyo inatokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kiangazi na ukame vikiwa ratiba ya kila mwaka maeneo nusu-jangwa na jangwani (Asal). 

Janet Oginga, licha ya umri wake mdogo ni miongoni mwa wakulima wanaojituma kuzalisha mimea inayohimili athari hasi za ukame.


Kilimo cha mihogo ndio mwajiri wa Janet Oginga. PICHA|SAMMY WAWERU

Janet, 23, hulima mihogo Rongo, Kaunti ya Migori.

Anasema, awali alikuwa akifanya vibarua vya kulimia watu mashamba na ni kupitia utangamano na mkulima aliyekuwa akikuza mihogo alishawishika. 

“Ninalima mihogo kwenye ekari mbili, na ikiwa kuna kazi nisiyojutia ni kuingilia ukuzaji wa zao linalostahimili mikumbo ya kiangazi,” Janet anasema, akidokeza kwamba 2024 utakuwa mwaka wake wa tano. 

Mimea mingine anayokuza ni pamoja na mahindi ya rangi; nyekundu na manjano, na mseto wa mboga za kienyeji. 

Cha kuridhisha katika kilimo cha mihogo ni kwamba hakina fomula yoyote wala kazi ngumu katika upanzi. 

“Ni mmea ambao ukipanda ni vigumu kushambuliwa na wadudu na magonjwa,” Janet anasema. 

Mbegu, ambazo ni matawi ya mihogo (cuttings), zinapandwa kwenye mashimo au mitaro. 

“Inachukua mwaka mmoja kukomaa na kuanza kuvuna,” adokeza. 

Mihogo huchimbwa au kung’olewa, sawa na viazi vitamu au nduma zinavyovunwa.

Janet Oginga akielezea wakulima kuhusu mimea asilia anayokuza wakati wa maonyesho ISFAA 2023. PICHA|SAMMY WAWERU

 

Mihogo ni kati ya mazao ambayo Serikali ya Kaunti ya Migori inahamasisha wakulima kuzalisha. 

“Kama serikali ya ugatuzi, tunahimiza wakulima kukuza mimea inayostahimili makali ya kiangazi na ukame. Kero ya njaa nchini, itakabiliwa wakulima wakijishirikisha kwenye ukuzaji wa mimea asilia kama vile mihogo, njugu na viazi vitamu, kati ya mingine,” anasema Lucas Mosenda, Waziri (CEC) wa Kilimo, Ufugaji, Samaki, Uchumi Samati na Vyama vya Ushirika katika Kaunti ya Migori. 

Kulingana na afisa huyu, Migori pia inahamasisha uongezaji thamani kupitia mifumo na teknolojia za kisasa. 

“Mapato ya kuridhisha, siri ipo kwenye uongezaji thamani. Kwa mfano, njugu karanga zikimiminwa mafuta, yatateka soko lenye ushindani mkuu sawa na kuunda vitafunio vya mihogo,” CEC Mosenda anaelezea.

Hatua hiyo, afisa huyu anasema inasaidia kupunguza mazao kuharibika na hata kuoza, ikizingatiwa kuwa wakulima wanakadiriwa kupoteza karibu asilimia 30 ya mazao msimu wa mavuno.

Kufuatia mabadiliko ya tabianchi, wakulima hasa wa maeneo kame wanahimizwa kukumbatia kilimo cha mimea inayostahimili makali ya kiangazi na ukame kama vile mihogo. PICHA|SAMMY WAWERU

Kupitia ufadhili wa Banseok Industry Company Ltd kwa ushirikiano na Korea Trade Investment Promotion Agency (Kotra), mwaka uliopita, 2023, Migori ilipokea msaada wa mashine tano kusaga njugu na kuongeza thamani.

Janet, anasema ni kwa muda tu aanze kuongeza mihogo thamani.

Kilimo chake ni cha kibiashara.

Mkulima huyu mchanga alikuwa miongoni mwa wakulima waliopamba Maonyesho ya Mbegu za Kiasili na Chakula cha Tamaduni za Kiafrika 2023, Makala ya Pili, yaliyoandaliwa na muungano wa Inter-Sectoral Forum on Agrobiodiversity and Agroecology (ISFAA).

ISFAA inaleta pamoja sekta za serikali na za kibinafsi katika kilimo, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, ya utafiti, na makundi ya wakulima kwa lengo la kilimo endelevu na kuboresha mazingira.

Kauli mbiu ya maonyesho hayo yaliyofanyika katika Makavazi ya Kitaifa – Kenya, Nairobi ilikuwa ‘Kuadhimisha Uhuru wa Chakula na Mbegu Nchini Kenya – Kufufua na kulinda Mfumo wetu wa Chakula na Kilimo huku tukikita Mizizi yetu, Kudumisha Mustakabali Wetu wa Kwanza’.