Safari ya barobaro singo aliyeanza ufugaji na kuku 3, sasa anamiliki maelfu
NA SAMMY WAWERU
KELVIN Kilonzo, ni mjasirimali ambaye amegundua kuna furaha na ufanisi katika ufugaji wa kuku.
Ni ari aliyoanza kupalilia akiwa mchanga kiumri, mfumo anaokumbitia ukiwa ni ule wa kuhakikisha walaji bidhaa za kuku wanazipata kwenye sahani kutoka ‘shambani’ moja kwa moja.
Huongeza thamani mayai anayozalisha kwenye mradi wake, kwa kuyaangua vifaranga.
Safari ya Kilonzo katika ufugaji kuku inaweza kufupishwa kwa kumtaja kama “mkulima aliyebaini alichotaka tangu utotoni”.
Akiwa alianzisha ufugaji akiwa Tala Machakos, ameufanikisha na kuufanya wenye manufaa.
Anadokeza kwamba akiwa mdogo, angetumwa na mamake kununua bidhaa sokoni au dukani hela zilizobaki alikuwa akiweka akiba.
“Kila sarafu ambayo mama alikuwa akinipa, nilikuwa nikiweka kama akiba. Shukran kwa ukarimu wake,” anasema.
Anaambia Taifa Leo Dijitali kwamba kwa mtaji wa Sh30, alianza na vifaranga watatu – ambao wameishia kuzindua mradi mkubwa.
Licha ya changamoto za hapa na pale, Kilonzo hakufa moyo.
Jitihada zake zilipelekea kuku kuongezeka mara dufu, kiasi cha kuwa mfadhili wa masomo yake katika shule ya upili.
“Kwa mfano, karo ya kidato cha tatu na cha nne, nilijilipia karo kupitia biashara ya kuku,” anafichua.
Baada ya kukalia Mtihani wa Kitaifa Kidato cha Nne (KCSE), alisomea Stashahada (Diploma) ya Masuala ya Wanyama akiegemea mafunzo ya kuku.
Hata akiwa katika taasisi ya elimu ya juu, Kilonzo aliendelea kuboresha biashara ya kuku huku akijumuisha ukuzaji mboga na nyanya.
Kilonzo kwa sasa ni kati ya wafugaji wa kupigiwa upatu nchini, akiwa na mradi mkubwa wa uanguaji mayai kupata vifaranga katika Kaunti ya Kiambu.
Chini ya kampuni yake ya Tala Poultry Farmers, vilevile, ana mradi wa kuku wa kutaga mayai ya kienyeji Kangundo Road, Machakos.
Nilianza kuangua vifaranga 200 na sasa nina maelfu, aelezea.
Aidha, ana viangulio (incubators) 20.
Wakati wa mahojiano, tulimpata akiwa na kuku 3, 000 wanaotaga mayai na idadi sawa na hiyo, 3, 000, ya vifaranga.
Kuku wake wakiwa ni wa kienyeji walioimarishwa, hufuga aina ya Kuroiler F1 (wenye asili ya India), Rainbow rooster, Sasso (Ufaransa), Kari, na Kenbrow.
“Nyakati zingine huangua hadi vifaranga 20, 000,” aelezea barobaro huyu ambaye angali singo.
Soko lake, ni mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), makundi ya vijana na kina mama kutoka Kaunti ya Machakos, Makueni, Nairobi, na Kiambu, ikiwa ni pamoja na wafugaji binafsi.
Isitoshe, husambazia hoteli na mikahawa kuku wa nyama.
Mradi wake wa Kangundo Road ukiwa ni wa uzalishaji mayai, anasema hukusanya karibu asilimia 85 ya bidhaa hiyo kwa siku.
Bei ya vifaranga inalingana na umri, wa siku moja akigharimu Sh100.
Aidha, kuku aliyekomaa bei yake ni kuanzia Sh800.
Huku wafugaji wakiendelea kulemewa na gharama ya juu ya malisho, Kilonzo amekumbatia mfumo wa kujiundia chakula cha kuku hatua ambayo wataalamu wanapigia upatu.
“Mfumko wa bei ya chakula cha mifugo ni kero ya kimataifa, na kwa mkulima anayetaka kusalia kwenye biashara kama vile ya ufugaji kuku hana budi ila kujiundia malisho,” Dkt Morris Irungu, mtaalamu, anashauri.
Ughali wa chakula cha mifugo umechochewa na ushuru wa juu (VAT) unaotozwa malighafi nchini na pia kuadimika kwa malighafi yenyewe.
Inakadiriwa Kenya huagiza kutoka nje zaidi ya asilimia 70 ya malighafi ya kutengeza chakula cha mifugo.
Kwa kujiundia chake, Kilonzo anadokeza kwamba amefanikiwa kupunguza gharama ya ufugaji kwa karibu asilimia 75.
Kwenye mradi wake, mfugaji huyu pia amekumbatia mfumo wa kisasa kunywesha kuku maji ambapo ndege hao hudona tapu zilizounganishwa na mifereji iliyosindikwa vizimbani.