Michezo

Salah kukosa mechi ya Misri dhidi ya Cape Verde kwa sababu ya jeraha

January 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

MOHAMED Salah atakosa mechi muhimu ya Kombe la Afrika (Afcon) kati ya taifa lake la Misri na Cape Verde katika ‘Kundi B’ kutokana na jeraha la paja.

Fowadi huyo mzoefu wa Liverpool atakosa pia gozi la hatua ya 16-bora kwenye Afcon iwapo Misri, ambao ni wafalme mara saba wa kipute hicho, watafuzu kwa raundi hiyo.

Salah, 31, aliondoka uwanjani akichechemea katika kipindi cha kwanza katika pambano lililoshuhudia Ghana wakiwalazimishia sare ya 2-2, Alhamisi.

Matokeo hayo yaliacha Misri katika ulazima wa kukomoa Cape Verde katika pambano lijalo ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele kutoka ‘Kundi B’ linalojumuisha pia Msumbiji ambao hawajawahi kushinda mechi yoyote kwenye fainali za Afcon.

“Vipimo vya afya ambavyo Salah amefanyiwa vimebaini kuwa ana jeraha la paja na hivyo atakosa mechi mbili zijazo za Afcon,” ikasema sehemu ya taarifa ya Shirikisho la Soka la Misri.

Ina maana kwamba Salah atanogesha tena gozi la Afcon kwa mara nyingine iwapo tu Misri watafuzu kwa robo-fainali zitakazosakatwa Februari 2 na Februari 3, 2024.

Misri walianza vibaya kampeni zao za ‘Kundi B’ kwenye Afcon nchini Ivory Coast baada ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Msumbiji kabla ya kutoka nyuma mara mbili na kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Ghana.

Misri walinyanyua taji la mwisho la Afcon mnamo 2010, mwaka mmoja kabla ya Salah kuvalia jezi za kikosi hicho kwa mara ya kwanza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO