Bambika

Oga Obinna ataka jamii kuwaonea huruma wanaume wanaochapwa kwenye ndoa

January 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA FRIDAH OKACHI

MCHEKESHAJI Steve Thompson Maghana almaarufu Oga Obinna ameshauri Wakenya kukoma kuwacheka wanaumme wanaopigwa na wake wao kwa kushindwa kulipa bili au sababu nyinginezo za kifamilia.

Alisema kuna wanaumme ambao wanashindwa kulipa bili kwa kukosa kazi au kazi wanayofanya ina mapato ya chini yasiyoweza kutosheleza mahitaji ya kinyumbani.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Obinna alipendekeza watu kukoma kuwacheka wanaumme ambao wanajitokeza kulalama kwamba wanafanyiwa dhuluma wakati wanashindwa kugharimia bili.

“Tuache kucheka wale wanaume wanaojitokeza na kusema wamepigwa ama wameshindwa kulipa bili fulani,” alichapisha Obinna.

Mchekeshaji huyo alisisitiza kwamba licha ya baadhi ya wanaumme kushushiwa kichapo, hawapati jamaa au rafiki wa kuwaelezea. Jamii inahukumu vikali.

“Wanaume wengi wamekuwa wakiumia kwa muda mrefu bila kuwepo na yule anayejali. Wengi wao wanajitia kitanzi kimyakimya. Wanaume hawana marafiki ambao watawapigia simu kuwaeleza matatizo yao,” aliongeza Obinna.

Obinna aliye na chaneli ya YouTube, alisema wanaume wanapigwa na wake zao na hakuna anayewatetea.

“Kuna huyu mwanamume aligundua mke wake ana mahusiano mengine nje ya ndoa… Naomba tuwajulie hali wanaume na mtoto wa kiume katika jamii,” akashauri.

Baba huyo wa watoto wanne alishauri kanisa, serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii kuzungumzia dhuluma kwa jinsia ya kiume pamoja na kuwezesha programmu za kuelimisha mtoto huyo.

Utafiti kutoka Idara ya Afya na Huduma za Binadamu, unaonyesha kuwa kati ya wanaume 1,000, asilimia 51.5 wanafanyiwa ukatili na wake au wapenzi wao wa karibu angalau mara moja katika maisha yao na asilimia 10.5  katika kipindi cha mwaka mmoja.