Jinsi wanawake Mlima Kenya wanahadaa vijana kwa pombe wawatunge mimba
NA MWANGI MUIRURI
WANAUME kutoka eneo la Kati mwa Kenya wanalalamikia mbegu zao za uume kuvunwa na wanawake pasi maafikiano.
Wametoa malalamiko hayo kupitia Baraza la Wazee, wakishangaa jinsi mbegu zao zinatumika kutungisha ujauzito.
Katika njama hiyo, wanawake ambao wameamua kuishi bila kujiingiza katika mikataba ya ndoa lakini wakiwa na haja ya kuzaa watoto wametajwa kulenga wanamume na kujiachilia hadi watungwe mimba.
Wanawake wengi siku hizi wakiwa na pesa zao, hupuuza ndoa wakizitaja kama utumwa wa kuhatarisha maisha yao kupitia uraibu wa ulevi, misukumo ya fujo kupitia utumizi wa mihadarati, aibu za kupigwa mnada kutokana na wanaume kuzama kwa kamari na pia mauaji ambayo yamezidi ndani ya ndoa.
Kusambaratika kwa ndoa kwa sababu ya umasikini, uraibu wa kujimaliza, kutowajibika na matatizo ya kiakili kumewaacha wanawake wengi wakihofia kuingia kwa mahusiano ya kudumu wakiamua tu kuwa wavunaji mbegu.
“Wakishapata mimba wanatafuta kijisababu cha kukatiza uhusiano huo, wanazaa na kulea watoto wetu pasipo kutuhusisha,” anasema Mzee Joseph Kaguthi ambaye kwa muda mrefu alihudumia taifa kama mkuu wa mkoa.
Bw Kaguthi alisema tetesi hizo zimewasilishwa na vijana wengi wa eneo hilo na ni mtindo ambao sasa umedhihirika kuwa umejipa mizizi ya kina.
Unasikia wanawake wakijiita singo lakini wana watoto ambao walivunwa kupitia hadaa.
Bw Kaguthi alisema kimila sio vyema kuvuna mbegu za mwanamume, hasa ukiwa wewe sio mkewe.
“Watoto wanaozaliwa kwa njia hiyo ya ukora huishia na masaibu tele maishani kwa kuwa hawana baraka za baba mzazi aliyeibwa mbegu zake na kisha akatemwa nje. Watoto hao ni kama tu mali ya wizi,” akasema.
Mwenyekiti wa baraza la wazee Bw Wachira Kiago alisema “ni vyema mtoto ajulishwe babake na ndiyo sababu ni hitaji la Bibilia na pia la itikadi za kimila kwamba watoto wazaliwe ndani ya ndoa”.
Aliteta kwamba kuna usasa na uzungu ambao umejipenyeza katika jamii ambapo mwanamke ananyemelea mbegu za mwanamume na kuzivuna bila huruma.
“Baadhi ya wanawake kwa kuwa wana pesa wanasaka vijana werevu na walioumbika vizuri, lakini ulevi umewateka nyara. Wanawanunulia pombe na kuwachezesha mzaha hapa na pale huku wakiwapa tunda na hatimaye wanashika mimba,” akasema Bw Kiago.
Anasema, “Ndio maana mitaani kumejaa watoto ambao unashtukia wanafanana na watu wenu lakini mama zao hawajawahi kuolewa katika familia zenu”.
Mzee Gathua Mwangi 94, kutoka Kaunti ya Kirinyaga anasema kwamba wizi huo wa mbegu umekuwa katika jamii tangu jadi.
“Enzi za wazazi wetu kulikuwa na kasumba za uchawi na kina mama walikuwa wanaogopa kurogewa watoto wao waage dunia wote. Walikuwa wakiamini kwamba ungebeba mimba ya nje ya boma na uzae mtoto, huyo angeokoka njama za warogi, na aishie kunusuru familia na kizazi,” akasema.
Alisema familia nyingi za Agikuyu zilikuwa na mtoto huyo wa nje kama kinga au bima dhidi ya uchawi na wenye mbegu hawakuwa wanaombwa ruhusa.
“Hiyo ndiyo tabia ambayo kwa sasa imegeuzwa kuwa ya kupata watoto pasipo ndoa. Huu ni ukora ambao tumekuwa nao katika historia na ni vile tu leo mnaona kama ni maajabu,” akasema.
Mzee Mwangi pia anahoji kwamba wanaume ambao wanajipata wamerushwa korokoroni kwa vipindi virefu na kuacha mabibi wachanga nyumbani, wanakwamisha maisha ya mahaba ya warembo wao.
“Ni wazi ikiwa una miaka 30 na umefungwa kifungo cha miaka 20 au 30 utarajie bibi yako avune mbegu za wanaume wengine ili ukitoka jela upate familia yako ikiwa imara,” akasema.
Alisema hakuna hatari ya wanaume kuvunwa mbegu kwa kuwa “hata kuna msemo miongoni mwetu ambao husema huwezi ukamnyima mtu mbegu ya kupanda”.