Tetesi kachumbari ya mayai chemsha na soseji mitaani inaundwa kwa nyanya zilizooza
NA SAMMY WAWERU
JE, wewe ni shabiki wa soseji, kebab au mayai chemsha yanayochuuzwa mitaani na kuongezwa ladha kwa kutumia kachumbari?
Hebu pata huu uhondo; Unaposhibikia vitafunio hivyo, huenda kachumbari unayotiliwa imeundwa kwa viungo vilivyooza.
Visa vya walaji wa mayai na soseji zilizowekwa kachumbari inayorusha uvundo vimeripotiwa katika mitaa kadha Kaunti ya Nairobi na viungo vyake.
Elvis, ambaye si jina lake halisi kwa sababu za kiusalama, anasema amejipata mara kadhaa akitiliwa kachumbari yenye shaka.
“Ninapenda mayai na soseji zilizowekwa kachumbari, na si mara moja, mbili au tatu nimetilia shaka baadhi ya wauzaji kufuatia viungo vinavyotoa uvundo,” Elvis ambaye ni mkazi wa mtaa wa Githurai anasema.
Hufanya kazi jijini Nairobi, na anasema majira ya mchana akiwa kazini na jioni hakosi kula mayai au soseji.
“Kisa cha kwanza, nilishuhudia mtaani Githurai kachumbari niliyowekewa kwenye yai nyanya zilikuwa na dalili ya kuoza. Hali hiyo si tofauti na ya kitovu cha jiji la Nairobi, ambapo nimejipata mara kadha kutilia shaka kiungio hicho,” anasema.
Kachumbari ni mchanganyiko wa nyanya, vitunguu na giligilani (dhania) zilizokatwakatwa kuwa vipande vidogo.
Hali kadhalika, viungo hivyo hutiwa pilipili hoho – ile kali kuongeza ladha zaidi.
Joshua, si jina lake halisi pia, mwenyeji Kariobangi anazua tetesi za aina hiyo.
“Usipokuwa makini, utaishia kula nyanya ambazo zimeharibika na kuoza,” Joshua anasema akikumbuka tukio ambapo alilumbana na mchuuzi wa mayai na soseji.
“Awali nilikuwa shabiki wa vitafunio hivyo vya haraka vinavyozima makali ya njaa ila siku hizi huwa mwangalifu sana,” Hellen, mkazi Mathare akaambia Taifa Leo Dijitali kupitia mahojiano kwa njia ya kipekee.
Jijini Nairobi (CBD) wachuuzi wa mayai, soseji, viazi karai na kebab wamesheheni.
Aidha, huuza bidhaa hizo kwa kutumia troli.
Sarah Muinde, mchuuzi wa bidhaa hizo zenye mashabiki wengi mitaani eneo la Zimmerman anashauri umuhimu mtu kula kwa muuzaji anayeona akiandaa viungo hivyo.
“Mimi huandamana na nyanya, vitunguu, dhania na pilipili ninazoandaa, na hukatakata wateja wangu wakiwepo,” anadokeza, akihimiza wachuuzi wenza kuwa wenye uwaazi.
Sheria ya Afya, hata hivyo, inahitaji wachuuzi wa bidhaa za kula mitaani wawe na leseni kuonyesha wameafikia vigezo vyote vya siha.
Wachuuzi aghalabu huweka troli zao kwenye vituo vya matatu, barabara zenye idadi ya juu ya watu na karibu na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kuteka wateja.