DeSantis ajiondoa na kuunga Trump kwa urais Amerika
FLORIDA, AMERIKA
GAVANA wa Florida, Ron DeSantis Jumapili alisitisha kampeni zake za kuwania urais kupitia chama cha Republican na kumuidhinisha aliyekuwa rais wa Amerika Donald Trump.
DeSantis alichukua hatua hiyo siku mbili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa mchujo katika jimbo la New Hampshire.
Hatua hiyo inafikisha kikomo azma ya Desantis ya kuingia White House baada ya kushindwa kukidhi vigezo ambavyo vingemfanya mpinzani mkubwa zaidi wa Donald Trump.
“Ni wazi kwangu kwamba wapigakura wengi wa mchujo wa chama cha Republican wanataka kumpa Donald Trump nafasi nyingine,” alisema katika hotuba aliyoitoa katika jimbo la New Hampshire, ujumbe sawa na alioutoa awali kupitia mtandao wa ‘X’ uliojulikana awali kama Twitter.
Aidha, DeSantis alimdhihaki Balozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa Nikki Haley, ambaye kwa muda mrefu alikuwa mpinzani wake wa karibu kwa nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha kutafuta tikiti ya chama hicho, akisema kwamba “hafai kuwa rais wa Amerika.”
Gavana huyo, ambaye amekuwa akionyesha shauku kubwa, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha urais wa 2024 akiwa na matumaini makubwa katika azma yake ya kumshinda Trump.
Hata hivyo, kura za maoni za awali zilionyesha kwamba alikuwa katika nafasi nzuri ya kufanya hivyo.
Yeye na washirika wake walichangisha zaidi ya dola milioni 100, na alijivunia rekodi yake ya kisheria kuhusu masuala muhimu kwa wahafidhina wengi, kama vile utoaji mimba na mafunzo ya masuala ya rangi na jinsia shuleni.
Wiki jana, alishindwa katika uchaguzi wa mchujo katika jimbo la Iowa – ambao alikuwa ameapa kushinda – kwa asilimia 30 dhidi ya Trump.
Hatua ya Desantis kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho sasa inawaacha Trump na gavana wa zamani wa jimbo la South Carolina, kushindania nafasi hiyo, siku moja kabla ya uchaguzi wa awali wa chama hicho katika jimbo la New Hampshire.