Habari za Kitaifa

Ruto sasa aahidi kutii maamuzi ya mahakama

January 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MARY WANGARI na BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto ameahidi kutii maagizo ya mahakama mradi tu athibitishe yametolewa na majaji ambao hawajahongwa.

Kiongozi wa nchi aliambia Jaji Mkuu kwamba japo hana shida kutii maagizo ya mahakama, baadhi yanalemaza ajenda za serikali yake na baada ya uchunguzi hubainika huwa yanatolewa na majaji wafisadi.

“Hatuna shida ya kutii maagizo ya mahakama, lakini baadhi yanatulemaza na tunapochunguza, tunabaini yanatolewa na majaji wanaohongwa,” alisema.

Alisema serikali yake itaheshimu utawala wa sheria na kutii maagizo ya korti lakini akasisitiza majaji wafisadi hawafai kulindwa.
Duru katika mkutano wa Rais Ruto na Jaji Koome katika Ikulu ya Nairobi jana zilisema mkuu wa mahakama alikiri kuna maafisa fisadi katika idara hiyo.

Mkutano huo ulileta pamoja wakuu wa mihimili mitatu ya serikali akiwemo Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Wakili wa Serikali Shadrack John Mose na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru, vilevile walihudhuria mkutano huo.

“Katika muda wa siku 30, kila tawi la serikali litawasilisha mapendekezo yaliyotolewa katika kikao cha NCAJ kinachoongozwa na Jaji Mkuu,” ilisema taarifa kutoka Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed.

Hatua hii huenda ikaashiria mwisho wa malumbano ya mara kwa mara baina ya serikali ya Rais Ruto na Idara ya Mahakama hususan kuhusu madai ya ufisadi.

Mapema mwezi huu, Dkt Ruto alizua hisia mseto baada ya kuishutumu vikali Idara ya Mahakama kwa kulemaza ajenda yake ya maendeleo kwa ushirikiano na makundi fulani ya mabwanyenye.

Huku akiwashutumu baadhi ya majaji kwa kuwa wafisadi, Rais alisisitiza kuwa atakiuka maagizo yanayotolewa kwa lengo la kuhujumu utekelezaji wa miradi muhimu kama vile Nyumba za Bei Nafuu na Bima ya Afya kwa Jamii (SHIF).

Akihutubia wanahabari Jumatatu wiki iliyopita, Bi Koome alifichua kwamba Idara ya Mahakama ilimwandikia Rais Ruto ikiomba kushiriki naye kikao kwa lengo la kutatua chimbuko la malalamishi ya Dkt Ruto dhidi ya majaji.

Mkutano

“Leo hii, kutokana na ombi lililowasilishwa na Idara ya Mahakama, Rais alileta pamoja viongozi wa Serikali, Bunge na Idara ya Mahakama katika kikao kujadili mikakati ya kupiga vita ufisadi, kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji huduma kwa Wakenya,” alisema taarifa kutoka Ikulu.

Taarifa ya Ikulu ilisema rais alikubali kuongeza mgao wa fedha unaotengewa Idara ya Mahakama katika juhudi za kuboresha utoaji huduma na vita dhidi ya ufisadi.

Nyongeza hiyo ya fedha itakayotekelezwa katika bajeti ijayo, itawezesha mahakama kuajiri majaji wapya 36 Mahakama Kuu (25) na 11 wa Mahakama ya Rufaa.