Wanafunzi 25 waliokosa KCPE kujiunga na shule za upili
NA GEORGE ODIWUOR
WANAFUNZI 25 waliokosa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE 2023) katika eneobunge la Homa Bay watajiunga na Kidato cha Kwanza, Wizara ya Elimu imetangaza.
Wanafunzi hao wataingizwa kwa shule mbalimbali za upili kulingana na alama walizokuwa wakifanya katika mitihani mbalimbali wakiwa katika shule za msingi.
Aidha Bi Osano alisema watapekuwa kuhakikisha wanafunzi hao walikuwa wakifuatilia masomo ya mtaala wa hapa nchini Kenya.
Kwa mujibu wa agizo la wizara, wanafunzi hao wanatarajiwa kufanya mtihani mwingine watakapokuwa katika Kidato cha Tatu kabla ya kuingia Kidato cha Nne. Mtihani huo utapewa hadhi sawa na KCPE.
Msichana ambaye alihudhuria masomo yake mwaka mzima lakini akakosa kufanya KCPE ni miongoni mwa watakaojiunga na shule ya upili chini ya utaratibu huo wa kipekee.
Shule yake ilikuwa na watahiniwa 190 lakini jina lake lilikosekana kwenye orodha.
Shule ilisema wanafunzi wote waliambiwa kuthibitisha majina yao.
Mwanafunzi huyo alikuwa akijificha kwa choo wakati wenzake walifanya KCPE kwa siku tatu.
Babake msichana huyo alishangazwa mno.
“Binti yangu aliniambia hakufanya mtihani wakati matokeo yalitangazwa,” akasema mzazi wa mtoto huyo.
Bi Osano naye aliongeza kwamba farakano baina ya wazazi ilikuwa sababu nyingine ya wanafunzi wengine kukosa kufanya mtihani kwani walitoroka.
Pia alisema yuko mwanafunzi aliyekosa kufanya mtihani kwa sababu ya ugonjwa kumlemea katika kipindi hicho.