Serikali yawinda waliopata ‘E’ kwenye KCSE
NA WINNIE ATIENO
WIZARA ya Elimu imeanza kuwasaka zaidi ya wanafunzi 48,000 ambao walipata alama ya ‘E’ katika Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) ili wajiunge na vyuo vya kiufundi na taasisi nyinginezo za masomo.
Katibu katika Wizara ya Elimu, Dkt Belio Kipsang jana alisema kuwa wanafunzi wote ambao walimaliza kidato cha nne na kuanguka mtihani, lazima wajiunge na vyuo vya kiufundi ambapo watasomea kozi mbalimbali za kazi za mikono.
Kwenye mahojiano jijini Mombasa, Dkt Kipsang aliyekutana na wadau wa sekta za elimu na usalama, alisema kuwa serikali iko makinifu kuhakikisha kuwa wote waliofanya KCSE wanajiunga na taasisi mbalimbali za masomo.
Dkt Kipsang alikuwa ameandaa mkutano huo kufahamu kiini cha ukanda wa Pwani kupata ‘E’ nyingi katika mtihani wa mwaka jana.
“Jinsi mnavyofahamu Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu alijitokeza na kusema hadharani kuwa tunastahili kuwafuatilia waliopata ‘E’. Walikuwa 48,000 ambao ni asilimia tano ya waliofanya KCSE,” akasema Dkt Kipsang.
Aliongeza kuwa wameanzisha ushirikiano na maafisa wa usalama ili waliopata ‘E’ nao wahakikishe wanaendelea na masomo yao badala ya kupuuzwa hapo awali.
“Tutajitahidi kushughulikia matatizo yanayosababisha wanafunzi wapate ‘E.’ Lazima tuhakikishe wazazi nao wanapata thamani ya uwekezaji wao katika elimu ya watoto wao. Watoto wetu nao lazima pia wanufaike kwa kupita mtihani,” akaongeza.
Kuhakikish idadi ya wanaopata ‘E’ inapungua, katibu huyo aliwaamrisha wakurugenzi wa elimu waendeleze ziara nyingi katika shule ili kufuatilia jinsi walimu wanavyowafundisha wanafunzi.
Ziara hizo kwa mujibu wa Dkt Kipsang, zitasaidia walimu kumaliza mtaala wao wa masomo kwa wakati. Pia alisema Wizara ya Elimu itashirikiana na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kupiga jeki sekta ya elimu.
Wanafunzi 48,174 walipata alama ‘E’ kati ya watahiniwa wote 899,453 ambao walifanya KCSE.
Bw Machogu alisema idadi ya juu ya watahiniwa ambao walikuwa wamepata ‘E’ ilikuwa ya juu na ya kuhofisha.
“Ninahisi uchungu kuwa idadi kubwa ya wanafunzi bado wanapata ‘E’ licha ya wizara kutumia mbinu za kusawazisha alama,” akasema Bw Machogu akiyatoa matokeo ya KCSE mapema mwaka huu. Maafisa kutoka Wizara ya Elimu sasa watashirikiana na wakurugenzi wa elimu nyanjani kuchunguza kwa nini waliopata ‘E’ ni wengi kisha wawasilishe ripoti yao.
“Hata hivyo, lazima mwalimu, mzazi na mtoto, kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa sababu hao wote ndio huwa shuleni na matokeo yanahusu kujitolea kwao,” akasema.
Alifichua kuwa serikali inatumia asilimia 30 ya rasilimali yake kukwamua sekta ya elimu (Sh650bn).
Dkt Kipsang alisisitiza kuwa lazima matokeo mazuri yapatikane.
“Tutakuwa na kikao na kupata majibu kuhusu changamoto mbalimbali. Walimu watakuwa wakishirikiana na maafisa wa wizara nyanjani na TSC ili kukumbatia mbinu za kuinua kiwango cha elimu nchini,” akasema.
Pia katibu huyo aliwahakikishia wazazi, wanafunzi na walimu kuwa serikali iko chonjo na itazishughulikia changamoto zote ambazo zinakabili shule ikiwemo miundombinu kama kukosa maabara na pia vitabu.