Makala

Mahangaiko Murang’a huduma za picha za MRI na CT scan zikisambaratika

January 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

WENYEJI na wakazi wa Murang’a wanaosaka huduma za picha za MRI na CT scan katika hospitali za eneo hilo wataendelea kuelekezwa hadi hospitali za kibinafsi au za umma zilizoko katika kaunti jirani baada ya mashine muhimu kuharibika.

Huu ni mwezi wa tatu mfululizo wa huduma hizo kusambaratika na kuwaacha wenyeji katika mahangaiko makuu, ikiwa na maana kwamba waathiriwa wa ajali za barabarani, uvamizi, kuvunjika viungo na pia wajawazito wanaohitaji picha za kujihakikishia usalama wa watoto walio tumboni, hawana afueni katika hospitali za kaunti yao.

Hali ni mbaya kiasi kwamba Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu amemtaka Gavana Irungu Kang’ata kuhakikisha huduma hizo zimerejeshwa mara moja.

Seneta wa Kaunti ya Murang’a Bw Joe Nyutu. PICHA | MAKTABA

Akiongea katika mji wa Murang’a mnamo Januari 17, 2023, Bw Nyutu alisema kwamba hilo ni suala la dharura ambalo halifai kungoja na heri mikakati mingine yote isimamishwe ili wagonjwa wahudumiwe kwanza.

Alilalamika kwamba huenda vifo vikaanza kutokea au ulemavu kiholela kutokana na hali ambazo zingezuiwa kupitia picha za kusaidia kubaini shida za kiafya kwa wagonjwa.

“Wagonjwa wetu wanalalamika kuhusu hitilafu ya mashine hizo za hospitali hasa ile kuu ya Murang’a. Ningekuomba utie bidii urejeshee wagonjwa hao huduma hizo za picha ili kuwaokolea pesa, muda na sisi tujivunie utawala wako,” akasema Bw Nyutu akimlenga gavana Kang’ata.

Kwa sasa, mahangaiko ni makuu na gharama za kimatibabu zimezidi kuenda juu.

Seneta Nyutu alisema binafsi “nimekosa jibu kwa wananchi ambao wananisukuma kuwaulizia huduma hizo zitarejea lini.”

Kwa upande wake, Bw Kang’ata kupitia mitandao yake ya kijamii mnamo Januari 17, 2024, alisema kwamba utawala wake unanuia kukarabati mitambo iliyofeli haraka iwezekanavyo.

Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata. PICHA | MAKTABA

Alisema kuna mashine za awali zilizokuwa zikitumika lakini zikabadilishwa na zile za kisasa na ambazo sasa ndizo zimeharibika “na hizo ndizo nitahakikisha zimekarabatiwa ili zisimamie hali kabla ya hizo za kisasa kuundwa”.

Alisema anaelewa kuna shida.

“Tunaomba wananchi wetu watuwie radhi huku tukitia bidii ya kurejesha huduma hizo. Tutajitahidi kujadiliana na serikali kuu ambayo iko na jukumu la kukarabati baadhi ya mitambo ambayo imezua changamoto hii huku nasi tukizidi kusaka mbinu za kulegeza makali ya uhaba huu wa huduma,” akasema Bw Kang’ata.

Hayo yakijiri, wagonjwa wa huduma hizo za picha walilalamika kwamba madaktari wa hospitali za umma Murang’a ndio sasa wanapokea wagonjwa katika hospitali zao za kibinafsi kwa ada za juu.

“Unapata daktari ambaye tunamlipa kwa ushuru wetu ndiye tena mmiliki wa hospitali ya kibinafsi na anatutibu kwa ada za juu licha ya kwamba tumelipa ushuru wa kutusaidia kupokea tiba nafuu katika sekta ya umma,” akasema mshirikishi wa haki za kibinadamu eneo hilo Bi Nyambura Kang’ethe.

Alidai gavana anapiga kampeni za jinsi anavyojenga hospitali mpya katika kila kona ya kaunti.

“Afahamu kwamba zile zilizoko zinakabiliwa na upungufu wa wauguzi, dawa na huduma muhimu kama za picha,” akaongeza.