Makala

AFCON: Marasta barani Afrika watamani fainali iwe baina ya Senegal na Cameroon

January 27th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

Marasta duniani wanajulikana kwa kupendana na kuweka amani licha ya kudhaniwa kuwa na mapenzi na bangi.

Rasta mmoja mwanasiasa nchini Kenya kwa sasa Bw George Wajackoyah anatamani fainali ya dimba la timu bora Afrika linaloendelea nchini Ivory Coast iwe kati ya marasta wa Senegal na Cameroon.

“Ningetamani sana turejelee mechi hiyo ya kusisimua iliyogaragaziwa katika uwanja wa Charles Konan Banny mnamo Januari 19, 2024 kati ya marasta wa Senegal na wale wa Cameroon. Ilikuwa mechi babake na pia mamake na hiyo ndiyo fainali murwa zaidi ningetaka kushuhudia iwapo itatimia,” akaambia Taifa Leo Dijitali.

Wajackoya hufahamika sana na injili yake ya kupendelea mmea wa bangi uhalalishwe nchini akisema una manufaa tele ya kiuchumi, licha ya kukemewa sana na waliokolea maadili ya kijamii na wasiopenda kujiroga ili mahanjam ya kimihadarati iwapande.

Mechi hiyo iliisha kwa manufaa ya Senegal iliyotandika Cameroon mabao 3-1.

Timu hizo zilikuwa zimewekwa katika kundi moja la C na ambapo Senegal iliibuka ya kwanza kwa kushinda mechi zake zote 3 na kupata alama 9 huku Cameroon ikiponyoka kibahati kwa kuzoa alama 4.

Tangu 2015, timu ya Senegal hunolewa na ‘rasta’ Aliou Cisse wa miaka 48 huku nayo ya Cameroon mrasta Rigobert Song naye aliyeanza kunoa timu za taifa lake kuanzia mwaka wa 2016 pia akiwa na miaka iyo hiyo 48.

Timu hizo mbili aidha ziko na bendera zilizo karibu kufanana licha tu ya mpangilio wa rangi na pia rangi ya nyota iliyochorwa juu ya bendera hizo.

Cameroon imechukua taji hilo la Afcon katika awamu za 1984, 2000, 2002 na 2017.

Kwa upande wake, Senegal imelitwaa taji hilo mara moja tu mwaka wa 2021.

Lakini kwa sasa timu hii ya Senegal imeimarika na ni miongoni mwa zile zinazopigiwa upatu wa kufanya vyema licha ya kuwa kandanda ni sawa na kamari ya pata potea.

Katika maisha ya timu hizo mbili, zimekutana mara 15 ambapo Senegal imeibuka bora kwa kuandikisha ushindi mara 7, kutoka sare mara tatu na kupoteza mara 5.

Timu hizo zilikutana kwanza Aprili 11, 1963 ambapo Cameroon ilipoteza 1-0 nayo mara ya mwisho ikiwa ni katika Afcon inayoendelea nchini Ivory Coast ambapo Senegal iliibuka mshindi kwa maholi 3-1.

Kabla ya wakutane kwa fainali iwapo hawatajipata pamoja katika robo na nusu fainali, ni lazima kwanza Cameroon iilaze Nigeria hapo Jumamosi mwendo wa saa tano usiku nayo Senegal iinyamazishe mwenyeji Ivory Coast mnamo Jumatatu saa tano usiku.

[email protected]