Pesa zinatiririka taratibu, MCSK yaambia wanamuziki
NA WANDERI KAMAU
SHIRIKA la Kusimamia Muziki Kenya (MCSK) limewarai wanamuziki nchini kuwa wenye subira, linapoendelea kuwatumia fedha zinazotokana na uchezaji wa miziki yao kwenye maeneo tofauti nchini, kama vile vyombo vya habari.
Mnamo Jumatatu, shirika hilo lilisema kuwa litakuwa likitoa fedha hizo kwa awamu, kinyume na hapo awali, ambapo lilikuwa likiwatumia pesa wanamuziki kwa wakati mmoja.
Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo, Dkt Ezekiel Mutua, shirika hilo litatoa fedha hizo kati ya Januari 25 na Machi 29.
Baadhi ya wanamuziki walieleza wasiwasi baada ya kutopokea pesa zao, hata baada ya shirika kuanza kutuma pesa kwa wanachama wake zaidi ya 16,000.
Shirika linalenga kutuma Sh20 milioni lilizokusanya kutokana na uchezaji miziki.
Hata hivyo, Dkt Mutua alisema kuwa mchakato wa kutuma pesa kwa watu 16,000 si rahisi, bali ni utaratibu utakaowahitaji maafisa wa shirika hilo kuhakikisha kuwa wale wanaotumia wametoa maelezo mazuri.
“Kwa wanachama wetu wapendwa, tangazo tulilotoa kwa umma lilieleza kuwa muda wa kutuma pesa zenu utakuwa kati ya Januari 25 hadi Machi 29. Kuwalipa wanachama 16,000 na kuhakikisha jambo hilo limefanywa kwa ukamilifu si rahisi. Hata hivyo, tumefanikiwa kuwalipa wanachama 6,000 kwa muda wa siku mbili. Matumaini yetu ni kwamba tutakamilisha zoezi hilo kabla ya siku ya mwisho,” akasema Dkt Mutua.
Akaongeza: “Msiwe na wasiwasi. Kile kila mwanachama anafaa kuhakikisha ni kuwa maelezo tuliyo nayo ni sahihi. Pia, kuna wale wanaolipwa kwa njia tofauti, kama vile kupitia benki au njia ya simu. Kila mtu atalipwa.”