Serikali yasambaza mbolea kwa tahadhari kuu
NA WANDERI KAMAU
SERIKALI mnamo Jumamosi ilizindua awamu ya pili ya mpango wa kusambaza mbolea ya bei nafuu nchini, huku ikiahidi kuepuka matatizo yaliyoshuhudiwa kwenye awamu ya kwanza ya usambazaji wa mbolea hiyo mwaka 2023.
Baadhi ya matatizo yaliyoshuhudiwa mwaka 2023 ni mchakato huo kutekwa na mabroka walaghai, ambapo walikuwa wakiongeza bei za mbolea hiyo kiholela, kinyume na bei iliyowekwa na serikali.
Usambazaji huo ulizinduliwa na Katibu katika Wizara ya Kilimo Paul Ronoh jijini Mombasa, ambapo alisema kuwa serikali imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kuwa mbolea hiyo inawafikia wakulima bila matatizo yoyote.
“Mbolea hii imepangiwa kuwafikia wakulima ikizingatiwa kuwa wengi wao wanajitayarisha kwa msimu wa upanzi,” akasema Dkt Rono.
Kwenye hafla hiyo, Katibu huyo alizindua usafirishaji wa tani 400,000 za mbolea kutoka maghala ya kampuni ya Export Trading Group, eneo la Bonje, jijini Mombasa.
Kwenye awamu ya kwanza ya usambazaji wa mbolea hiyo, mchakato huo ulikumbwa na matatizo mengi, baadhi yakiwa wakulima kulalamika kutofikiwa na mbolea hiyo.
Baadhi ya wakulima walilalama pia kwamba majina yao hayakuwekwa kwenye orodha ya watu ambao walistahili kupata mbolea hiyo ya bei rahisi.
Serikali ya Rais William Ruto ilitangaza kupunguza bei ya mbolea kutoka Sh7,500 hadi Sh2,500 mara tu baada ya kuchukua uongozi, kwenye mikakati ya kuongeza uzalishaji miongoni mwa wakulima.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Dkt Rono alisema kuwa mbolea hiyo ni ya kiwango cha juu na itauzwa kwa Sh2,500 kwa gunia la kilo 50.
Alisema kuwa serikali itasambaza karibu magunia 7.5 milioni ya mbolea kwa wakulima kote nchini hadi pale msimu wa mvua utakapoanza.
Kinyume na hali ilivyokuwa kwenye awamu ya kwanza ya usambazaji huo, Dkt Rono alisema wataongeza vituo na maeneo ambao wakulima watakuwa wakichukua mbolea hiyo.
“Kwenye awamu ya kwanza, wakulima wengi walilalamikia uhaba wa maeneo ya kuchukulia mbolea hiyo. Tulisikia vilio vyao. Hivyo, katika awamu hii, moja ya hatua ambazo tumechukua ni kuongeza maeneo ambako watu watakuwa wakichukulia mbolea hiyo,” akasema.