Kibarua kizito Murang’a kinachomsubiri kamishna Joshua Nkanatha
NA MWANGI MUIRURI
KUMEZUKA furaha katika Kaunti ya Murang’a kufuatia kuhamishwa kwa Kamishna Patrick Mukuria.
Bw Mukuria alipewa uhamisho hadi Kaunti ya Kisii, Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu akisema kwamba “tunashukuru na tunashabikia uamuzi huo kwa kuwa kuna mambo mengi yalienda mrama katika uongozi wake”.
Bw Mukuria aliteuliwa kuwa Kamishna wa Murang’a baada ya Bw Karuku Ngumo kuhamishiwa Kaunti ya Wajir mnamo Machi 7, 2023.
Kwa sasa, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amemtuma Joshua Nkanatha kuwa Kamishna mpya wa Kaunti hiyo.
Bw Nyutu alisema: “Sasa ni kazi kwa Kamishna mpya awajibikie kero ya mauaji kiholela, pombe za mauti, upenyo wa soko la mihadarati, wizi wa mifugo, kelele za baa katika makao ya makazi na pia ufisadi katika sekta za huduma hasa polisi na afisi za mashamba”.
Muungano wa wazazi na wathamini wa shule katika Kaunti hiyo Bi Susan Kamande alisema kwamba “tulijaribu kumwelezea Bw Mukuria azime utundu wa baa lakini hata zile wadogo wake walifunga kwa msingi wa kuwa hatari kwa usalama wa eneo, ziliishia kufunguliwa kwa amri ya wakubwa”.
Bi Kamande aliteta kwamba kila kuchao Bw Mukuria alikuwa akiombwa azime kelele za mabaa za usiku katika maeneo ya makazi ambazo huathiri afya ya watoto.
“Sisi kama wazazi tumeshabikia hatua ya Waziri Kindiki ya kumhamisha Bw Mukuria. Ni mtu mzuri sana lakini kikazi ako na shida,” akasema.
Kabla ya Bw Mukuria kuteuliwa kuwa Kamishna wa Murang’a, alikuwa awali akihudumu kama katibu wa Kaunti hiyo chini ya Utawala wa Gavana wa kwanza, Mwangi wa Iria.
Katika kero la utundu wa mabaa, Bw Mukuria alikuwa akijitetea kwamba serikali ya Kaunti ikiongozwa na gavana Irungu Kang’ata ndiyo ilikuwa ikitoa leseni kiholela hivyo basi kutatiza utekelezaji wa sera za serikali kuu ambayo imeamrisha baa zipunguzwe na pia walanguzi wa mihadarati wasakamwe.
Kwa upande wake, Bw Kang’ata amekuwa akijitetea kwamba afisi ya Kamishna ndiyo ilikuwa ikikwepa jukumu la utekelezaji.
Rais wa muungano wa mawakili katika Kaunti ya Murang’a Alex Ndegwa alisema kwamba kumejaa matapeli wa mashamba wengi wao wakiwa na uhusiano wa moja kwa moja na baadhi ya wakuu wa kiutawala.
Ni katika utawala wa Bw Mukuria ambapo Naibu wa Kamishna wa Ithanga Kakuzi Bi Angela Makau alinaswa peupe akiwa na mitambo ya sola iliyokuwa imeibwa kutoka kwa mradi wa umma wa maji ambayo ilikuwa imefichwa katika jumba lake la kibinafsi.
“Kesi hiyo ilifichwa na hatimaye kile kilifanyika ni kupewa tu uhamisho na hadi leo mitambo hiyo haijarejeshewa umma,” akasema mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu eneo hilo Bw Romano Kang’ethe.
Pia, Machifu kadha wamehusishwa na njama za kuandaa kesi za kutatua mizozo ya mauaji na pia ubakaji.
Bw Kang’ethe aliongeza kwamba kero lingine kuu ni mauaji kiholela ya vijana katika mashamba ta ya Del Monte na Kakuzi lakini utawala wa Murang’a ukikosa kuingilia kati.
“Pia, Bw Mukuria alikuwa katika hatamu za uongozi wa Murang’a wakati kamati ya usalama ya Mathioya ilirekodi visa vingi vya maafisa wa polisi kuhusishwa na mauaji ya raia, kushambuliwa kwa raia na pia kutoweka kwa baadhi yao kama Esther Ruguru aliyeonekana mara ya mwisho Julai 1, 2023, katika Mji wa Kiria-ini,” akasema Bw Titus Kiai.
Askofu Edward Nyutu wa muungano wa dini asili alisema kwamba “Murang’a kulikosa adabu za kimsingi polisi wakionekana wazi wakichukua hongo kwa mabaa kuanzia saa mbili za usiku wakitumia magari rasmi”.