Kawira Mwangaza alivyochuuza nyanya 2013 baada ya kukosa kiti cha ubunge
NA MWANGI MUIRURI
GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza anasema kuwa alipoamua kujitosa katika ulingo wa kisiasa mwaka wa 2013 akiwa na umri wa miaka 34, alijua waziwazi kwamba alikuwa akiingia katika kinywa cha mamba.
“Niliwania kiti cha eneobunge la Buuri katika uchaguzi huo wa 2013 na nikaangukia pua. Kisha nikaenda Nairobi nilikoanza kuchuuza nyanya, kitunguu na viazi baada ya kampeni kunimalizia pesa,” asema.
Anasema kwamba kampeni zilimgharimu Sh20 milioni na akaanguka huku machungu na kusononeka yakihatarisha hata uhai wake wakati huo.
Mwaka wa 2017 alirejea ugani akiwania wadhifa wa mwakilishi wa Kaunti ya Meru na safari hii akafanikiwa kuutwaa.
Mwaka wa 2022 ndio aliamua kumenyana na miamba wa kisiasa ambapo aliwindana na mzee mzoeefu Kiraitu Murungi na Mithika Linturi na akawashinda.
“Katika chaguzi hizo mbili, nilikuwa nawania kama mwaniaji wa kujitegemea asiye na ufadhili wa chama…Na nikashinda,” asema.
Sasa, anasema kwamba siri yake ni Yesu ambaye katika imani yake ya Kikiristo humwongoza katika mawimbi ya miradi yake.
“Mimi ni askofu katika kanisa langu na ambalo huhubiri neema za Mungu. Katika maombi yangu, huwa namsihi Mungu anijalie mema na makubwa katika maisha ili niwe sauti na nguvu ya mnyonge wa kijamii,” asema.
Anasema kwamba “mimi hulia machozi nikimuomba Mungu anipe rasilimali ili niendelee kuokoa wengi kutoka lindi la umasikini na ndipo nikapewa ufunuo kwamba nyota yangu katika uongozi haingezimika”.
Alisema ana mkataba na Maulana wa kwamba “ukinipa yangu Mungu nitatengea waja wako ili nao wapate neema zako katika maisha yao”.
Bi Mwangaza anasema kwamba “hadi sasa mkataba wangu na Mungu ungalipo na amenipa hakikisho katika ufunuo kwamba sijafika mwisho, kwamba ana safari ndefu ambayo atanifanikishia katika uongozi”.
Katika hali hiyo, anasema kwamba “wale ambao wanajaribu kuning’atua, kuniharibia jina, kunihusisha na kashfa na pia kunivunja moyo waelewe kwamba wanayepigana naye ana ngome yake katika imani ya Maulana na hatatikisika”.
Ameteta kwamba “baadhi ya wanaonipiga kisiasa ni madalali huku wengine wakiwa ni makuhani wa ukandamizaji wa nyota za wengine”.
Bi Mwangaza alisema kwamba “itahitaji Mungu anikatae ili njama zenu zifanikiwe na kwa kuwa nina mkataba wa moja kwa moja na Mungu na pia watu wake, mtateseka kuniangamiza”.
Bi Mwangaza anasema kwamba “Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua walielewa kwamba Mungu amejiangaza Meru na wakakubali hali hiyo”.
Alisema kwamba hao wawili wamekuwa marafiki wa dhati katika dhiki zake, “nami pia nikizidi kumuomba Mungu awaguse nyoyo wapinzani wangu waelewe kwamba kuna wanyonge ambao wanafaa kuhudumiwa kwanza kabla ya tumenyane kisiasa 2022”.
Alisema kwamba “siasa zinazochezwa na baadhi ya wanasiasa wa Meru ni zile za matusi na dharau kwa msingi wa jinsia wala sio kwa maadili ya kiutawala”.
Hatimaye, anasema “tutakutana kwa debe 2027 na Mungu amenifunulia kwamba nitakuwa gavana miaka 10 na kisha anipe nyota nyingine ya kupaa zaidi”.
Alisema kwamba “kwa sasa nikiwa na miaka 44 ina maana kwamba 2027 tukimrejesha Ruto mamlakani kwa awamu ya pili nitakuwa na miaka 47. Mwaka wa 2032 nitakuwa na miaka 52 na nitakuwa nimeiva kuwa hata spika wa bunge la kitaifa au la seneti na Mungu akipenda zaidi, hata niwe Rais baada ya tulio na wao kwa sasa kuafikia awamu zao”.