Nakhumicha ateua kamati ya mpito kutoka NHIF hadi SHIF
NA CHARLES WASONGA
SERIKALI imebuni kamati maalum ya kukagua mali ya Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF), madeni yake, pensheni na malipo mengine ambayo inadaiwa kabla ya kuvunjwa kwake baadaye mwaka huu 2024.
Nafasi yake itachukuliwa na Hazina ya Afya ya Jamii (SHIF) ambayo sheria ya kuibuni sasa imehalalishwa rasmi na mahakama.
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alisema kuwa kamati hiyo itakayoongozwa na Kap-Kirwoka Jason itafanikisha mpito kutoka NHIF hadi SHIF.
Kamati hiyo ya watu 10 pia inajumuisha Bw Daniel Mwai, Bw Kipruto Chermusoi Chesang, Bi Jacinta N. Wasike, Bi Gladys Wambui Mburu, Bw Stephen Kaboro Mbugua, Bi Elizabeth Wangia, Bw Christopher Leparan Tialal, Bw Jacob Otachi Orina, na Bw Stanley Bii.
“Umma unajulishwa kwamba Waziri wa Afya ameteua Kamati ya Mpito kuhusu Mamlaka ya Afya ya Jamii itakayosimamia hazina ya SHIF ili kufanikisha mpito kutoka hazina ya NHIF,” likasema tangazo kwenye Gazeti Rasmi la Serikali toleo la Januari 25, 2024.
Wajibu mkuu wa kamati hiyo ni kusimamia kuvunjwa kwa NHIF kwa kuandaa kanuni zifaao.
Wanachama wa kamati hiyo pia watatoa ushauri kuhusu masuala mengine yanayohusiana na shughuli hiyo.
Kulingana na sehemu za mpito katika Sheria ya Hazina ya Bima ya Afya ya 2023, kamati hiyo pia inapaswa kuandaa mwongozo na mikakati ya utendakazi wakati wa mpito huo ili isaidie wakati wa ukaguzi wa hesabu, kuthibitisha uhamisho wa mali, wafanyakazi, pensheni na malipo mengine kwa wafanyakazi wa NHIF hadi hazina ya SHIF.
Kamati hiyo pia itabuni sheria maalum itakayosimamia uhamisho huo huku ikihakikisha kuwa umma unaendelea kupokea huduma.
Kamati hiyo itakagua ripoti rasmi, sera, sheria na stakabadhi nyingine husika.
Wanachama wa kamati hiyo pia wanawake kushirikisha wataalamu, haswa katika nyanja zenye uhitaji, itakavyohitajika.
Kamati hiyo ya Kap-Kirwok itahudumu kwa miezi sita na itawajibika kwa Waziri Nakhumicha, mwenyekiti wa bodi ya mamlaka inayosimamia SHIF na mwenyekiti wa Bodi inayosimamia NHIF.
Sekritariati ya kamati hiyo itahudumu katika Afisi za Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Wajibu wake utakuwa kufasiri sera, kuunda na kutekeleza mipango ya kamati hiyo huku ikitoa maelezo ya kila mara kwa kamati hiyo.
Baada ya Mahakama ya Rufaa kuweka kando agizo lililoharamisha utekelezaji wa Sheria ya hazina ya SHIF, Wizara ya Afya imekuwa ikijizatiti kuhakikisha kuwa kanuni za kufanikisha utendakazi wake zinakuwa tayari.
Sheria hiyo ilitungwa Novemba 2023 na kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali na waziri Nakhumicha.
Sheria hiyo inabuni Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) itakayoongozwa na Mkurugenzi Mkuu na Mwenyekiti.