Timamy mbioni kuinua uvuvi Lamu, Sh66m zikitolewa kufadhili miradi
NA KALUME KAZUNGU
SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imeanzisha harakati za kuinua sekta ya uvuvi na uhifadhi wa mazingira na jamii, ikiwemo kufadhili miradi sawia na hiyo ya kima cha Sh66 milioni.
Gavana wa Lamu Issa Timamy alipozuru ngome kuu ya uvuvi ambayo ni Lamu Mashariki, alifadhili karibu makundi 33 ya uvuvi, yale ya kijamii na uhifadhi wa mazingira ili kufanikisha azma yao, ikiwemo kuinua uchumi na maisha ya wakazi.
Miongoni mwa makundi yaliyonufaika ni sita ya wavuvi yaliyoko kisiwa cha Faza ambayo yalipokea vifaa vya kisasa vya kutekelezea uvuvi wao.
Vifaa hivyo vinajumulisha maboti sita na injini zao yatakayowawezesha wavuvi kuzamia uvuvi wa maji ya bahari ya kina kirefu.
Pia walipokea nyavu, misipi na ndoano miongoni mwa miundomsingi mingine.
Ufadhili huo unatekelezwa na serikali ya kaunti ya Lamu kwa ushirikiano na Benki ya Dunia (WB) kupitia mradi wake wa kufadhili Miradi ya Uvuvi na Maendeleo ya Kijamii Kenya (KEMFSED).
Mradi huo unanuiwa kuboresha Masuala ya usimamizi wa miradi ya uvuvi iliyoko ya kipaumbele ili kuinua ucumi na maisha ya wavuvi kwa ujumla kwenye ukanda wa Pwani.
Akizungumza eneo la Mtanawanda wakati wa kukabidhi maboti kwa wavuvi na wanajamii, Bw Timamy alisema ufadhili huo wa kaunti kwa ushirikiano na KEMFSED utawezesha kuzidisha usalama wa chakula na kukabiliana na ata kuondoa umaskini, hasa kwenye maeneo ya mashambani.
“Mradi huu unanuia kuongeza kipato katika kila nyumba. Mradi wenyewe unaenda sambamba na ajenda ya utawala wangu ya kuhakikisha uvuvi na shughuli za kilimo zinaboreshwa eneo hili kwa manufaa ya jamii yetu,” akasema Bw Timamy.
Wakati wa hafla hiyo, Bw Timamy pia alikabidhi vyeti na leseni kwa manahodha 15 wanaohudumu kwenye Bahari Hindi Kaunti ya Lamu.
Wavuvi wapigambizi 55 pia walikabidhiwa seti za kutekelezea shughuli zao baharini.
Baadhi ya wavuvi hawakuficha furaha yao baada ya kunufaika na ufadhili huo wa miundomsingi ya uvuvi.
“Twashukuru kwa msaada tuliopokea. Utapiga jeki shughuli zetu baharini na hata kupanua vilivyo sekta hii,” akasema Mohamed Omar.
Walioandamana na Bw Timamy kwenye hafla hiyo ya kuwakabidhi wavuvi na jamii vifaa ni Naibu wa Gavana, Raphael Munyua, Katibu wa Kaunti ya Lamu Ali Abbas, Msimamizi wa Idara za Kaunti, Abdulbasir Issa, mawaziri na mshirikishi wa miradi ya KEMFSED Kaunti ya Lamu Kamalu Shariff.