Mbunge wa Maragua kuendea maji ya wakazi Ikulu
NA MWANGI MUIRURI
MBUNGE wa Maragua Mary Wamaua ametisha kwamba atalazimika kuongoza maandamano ya wapigakura wake hadi Ikulu ya Nairobi kudai maji kutoka kwa Rais William Ruto kufidia ukosefu wa maji safi katika eneobunge lake.
Bi Wamaua alidai kwamba serikali ya Kaunti ikiongozwa na gavana Irungu Kang’ata inahujumiwa katika utendakazi wake wa kuafikia malengo ya maji safi ya kunywa na pia yale ya kushirikisha kilimo cha unyunyiziaji.
Katika kikao cha Januari 28, 2024, na wadau wa maji ya Maragua katika Mkahawa wa Golden Plan mjini Kenol, Bi Wamaua aliteta kwamba kampuni ya Maji ya Murang’a Kusini (Muswasco) ambayo hutoa huduma zake katika maeneo bunge ya Kandara, Kigumo na Maragua, hubagua eneobunge lake.
“Ni kwangu tu ambapo usambazaji maji safi umesimamia chini ya asilimia 20. Katika maeneobunge hayo mengine, kiwango chao cha maji safi katika mifereji kiko juu ya asilimia 70,” akasema.
Bi Wamaua aliteta kwamba licha ya eneobunge lake kuwa sawa na jangwa kutokana na ukame, “miundombinu ya maji ya unyunyiziaji iko katika kiwango cha chini ya asilimia tano licha ya kuwa sisi ni wenyeji wa mabwawa ya maji ya zaidi ya Sh2 bilioni”.
Aliteta kwamba bodi ya uratibu wa rasilimali za maji nchini (Wasreb) ilikuwa kati mwa mwakia jana imeagiza kampuni zote za huduma za maji katika Kaunti ya Murang’a zijisalimishe kwa usimamizi wa serikali ya Kaunti “lakini Muswasco haikutii mwelekeo huo na imebakia kuwa sawa na shirika la serikali kuu”.
Mbunge huyo alisema kwamba ushawishi wa aliyekuwa Waziri wa Maji wakati huo Bi Alice Wahome ndio ulichochea kampuni hiyo ikaidi wito huo wa kujisalimisha kwa kaunti.
Hata sasa wakati mikoba ya wizara hiyo imekabidhiwa Bw Zachariah Njeru kama Waziri wake baada ya Bi Wahome kuhamishiwa hadi wizara ya Mashamba na Majumba, Bi Wamaua akaongeza, “ameiga tu mtazamo wa Bi Wahome na hakuna analofanya kuwajibisha Muswasco kutii wito wa kisheria”.
Hata hivyo, Bi Wahome na Bw Njeru walikanusha madai ya kuchochea ukaidi kwa sheria wakisema kwamba “kuna mikakati iliyowekwa na pia kuna ukadiriaji wa miundombinu katika hatua za kushinikiza kubadili hali ya umiliki wa Muswasco”.
Bi Wamaua alisema kwamba baada ya kampuni zingine kutii mwito wa kuwa chini ya uratibu wa serikali ya Kaunti, gavana Kang’ata alikuwa ametoa idhini kwa kampuni ya Murang’a Kusini kwa jina Muwasco isaidie Muswasco kusambaza maji katika eneo bunge la Maragua.
“Lakini cha kukera zaidi ni kwamba, wakati wananchi hao wameanza kusambaziwa maji na Muwasco, bodi ya Wasreb imeandika barua ya kusitisha harakati hizo,” akasema.
Aliongeza kwamba hali hiyo imemuacha na aibu machoni kwa wapiga kura wake hivyo basi kumuchochea aandae maandamano hadi kwa rais “ambaye ndiye tulipea kura zetu za kutusaidia utekelezaji wa Katiba ambayo inadai haki za kila Mkenya kuboreshewa maisha yake”.
Aliteta kwamba “sijui vile Wasreb na Muswasco hutekeleza huduma zao ikiwa wanaweza wakazima wananchi kuunganishwa na maji”.
Hata hivyo, mkurugenzi wa Wasreb Bw Julius Itunga alisema suala hilo litatatuliwa katika mkutano ambao ameitisha ukiwaleta pamoja serikali ya Kaunti, Muswasco na Muwasco.
Walioitwa katika mkutano huo ni waziri wa maji wa Kaunti Bi Mary Magochi, Mkurugenzi mkuu wa Muswasco Bi Mary Nyagah na Mkurugenzi mkuu wa Muwasco Bw Daniel Ng’ang’a.
“Nimeita watatu hao katika mkutano wa majadiliano ili tuone jinsi mzozo huo unavyoweza ukasuluhishwa pasipo kuumiza mwananchi,” akasema.
Alisema mkutano huo utakuwa wa kupendekeza kupigwa msasa kwa mipaka ya kuhudumiwa na makampuni hayo mawili na pia suala la Muswasco kukaidi kuwa chini ya utawala wa Kaunti.
“Mkutano huo ni wa Januari 30, 2024 katika afisi zetu jijini Nairobi na wote wamethibitisha kuwa watafika. Tutapata mwelekeo na suala hili litatatuliwa kwa kuwa hata rais amekuwa akiongea kulihusu katika mikutano yake ya kikazi katika kaunti ya Murang’a,” akasema Bw Itunga.
Bi Wamaua alisema kwamba “wakutane au wasikutane mimi kile tu nataka kuona ni wapiga kura wa kwangu wakiunganishwa na maji safi ya kunywa ili waepukane na magonjwa hatari yanayotokana na utumizi wa maji machafu”.
Aidha, alisema eneo bunge lake hutegemea chakula cha misaada kutokana na mazingira yake ya ukame “na ningetaka kuona wakulima wangu wakiunganishwa na maji ya kushiriki kilimo ili tutafute utoshelevu wa chakuka cha lishe na pia cha kushirikisha biashara”.
Akitoa makataa ya wiki mbili suala hilo liwe limetatuliwa Bi Wamaua alisema kwamba “la sivyo mimi nitaongoza zaidi ya watu 2,000 hadi Ikulu Nairobi rais akatwambie maji yetu yako wapi na tiliahidi wananchi hawa kuwafanyia haki tulipokuwa tukiwaomba kura za ushindi wa 2022”.