• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wanawake watengewa nafasi 160 pekee kwenye jeshi

Wanawake watengewa nafasi 160 pekee kwenye jeshi

Makurutu wengi waliojitokeza kutafuta nafasi ya kusajiliwa kuingia jeshini watemwa katika awamu ya mapema kutokana na kukosa uzani uliostahili ili wajiunge na kikosi hicho. Wengi waliojitokeza walikuwa na kilo 49 kwenda chini kinyume na kilo 54.4 kwa wanaume na 50 kwa kina dada kama ilivyotakikana. Hapa ni Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Na CECIL ODONGO

Kwa Muhtasari:

  • Luteni Kanali Steve Kiago asema kwa kuwa nchi nzima kunahitajika makurutu wa kike wasiozidi 160
  • KDF mwaka huu inatarajia kuwasajili makurutu 2,000
  • Visa vya utoaji hongo vimepungua mno tangu usajili wa mwaka wa 2013
  • Vigezo ni  hali nzuri ya kiafya, alama ya D KCSE, miaka 18 hadi 26, kutokuwa na rekodi ya uhalifu na kitambulisho cha kitaifa
  • Wanawake wenye mimba watakaoripoti kwenye vituo vya kuwania kusajiliwa watafungiwa nje

WANAWAKE waliojitokeza Jumatatu katika uwanja wa michezo wa Nyahururu kwenye usajili wa makurutu wa jeshi, waliambulia patupu walipojulishwa kuwa hakukuhitajika hata mwanamke mmoja katika kituo hicho cha usajili, kaunti ya Laikipia.

Luteni Kanali Steve Kiago aliyeongoza usajili huo, alisema kwa kuwa nchi nzima kunahitajika makurutu wa kike wasiozidi 160 na kuwa, hakukutengewa nafasi ya wanawake eneo hilo.

Mmoja wa waliojitokeza, Bi Alice Wambui, alisema alivunjika moyo kwa kuwa ni mara yake ya tatu kufika kwa usajili na kufahamishwa kuwa hakuhitajiki wanawake.

“Umri unasonga na sijafanikiwa kusajiliwa. Hata hivyo, natumai mwaka ujao watasajili wanawake hapa petu,” akasema.

Shughuli ya usajili huo ilizinduliwa jana na Naibu Mkuu wa Majeshi Luteni Jenerali Joseph Kasaon ambaye alisema shughuli hiyo itakayodumu kwa mwezi itaendeshwa katika kaunti ndogo 320 kote nchini.

Kulingana na kamanda huyo, KDF mwaka huu inatarajia kuwasajili makurutu 2,000.

Wanaotaka kujiunga na jeshi watalazimika kupitia uchunguzi wa kiafya na vyeti vyao kukaguliwa kuhakikisha kwamba ni halali.

 

Uwazi

Jenerali Kasaon, ambaye aliandamana na msimamizi wa usajili huo Brigedia Joakim Mwamburi alisema watakaofaulu kuchukuliwa watatakiwa kuripoti katika Chuo cha Mafunzo ya Jeshi kilichoko Eldoret pindi tu usajili utakapokamilika.

“Tunataka shughuli hii iwe na uwazi ndiposa tunawaalika EACC, NSIS, Transparency international na hata wanahabari ili wawe waangalizi kwenye mchakato huu wa usajili,” akasema Luteni Jenerali Kasaon.

Alitaja kwamba visa vya utoaji hongo vimepungua mno tangu usajili wa mwaka wa 2013 na kuwapongeza mno Wakenya kwa hatua hiyo.
“Mwaka jana kulikuwa na visa vitano pekee vilivyohusisha Sh2 milioni jambo linaloashiria upigaji wa hatua mkubwa katika kukabiliana na kero la hongo,” akaongeza.

Baadhi ya kaunti ambapo shughuli hiyo imeanza ni Kiambu, Kisumu, Nyeri, Busia na Kwale huku vijana wachache wakijitokeza.

 

Hofu

Usajili wa maafisa wa polisi unaokuja baadaye umetajwa kuwa sababu kuu ya idadi hiyo ndogo huku wengi wakihofia kujiunga na jeshi kutokana na hofu ya kutumwa kuhudumu maeneo hatari kama vile Somalia.

Baadhi ya vigezo vilivyozingatiwa kwenye usajili huo ni mshiriki kuwa katika hali nzuri ya kiafya, alama ya D KCSE, miaka 18 hadi 26, kutokuwa na rekodi ya uhalifu na uwe na kitambulisho cha kitaifa.

Wanawake watakaoripoti kwenye vituo vya kuwania kusajiliwa watatakiwa kutokuwa na ujauzito. Pia usajili huo utazingatia sheria ya jinsia huku wanawake wakitarajiwa kutwaa theluthi mbili za nafasi hizo.

Usajili huo unatarajiwa kuendelea Jumanne kwenye vituo kadhaa katika kaunti za Meru, Kitui, Machakos, Kirinyaga na Embu huku idara ya jeshi ikitumai wengi watajitokeza kuwania nafasi ya kuhudumia taifa lao.

You can share this post!

Baba ajiua baada ya kukosana na mwanawe

Wakili wa Miguna kizimbani kwa dai alihepa ‘vuta pumzi’

adminleo