Junior Starlets wajifua kwa mechi dhidi ya DRC
Na TOTO AREGE
TIMU ya Kenya ya Wasichana chini ya umri wa miaka 17 almaarufu Junior Starlets, inaendelea kujifua kwa maandalizi ya mechi ya raundi ya pili ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mwezi ujao.
Raundi ya kwanza itachezwa DRC siku ya Jumapili, ikifuatiwa na raundi ya pili nyumbani tarehe Februari 11, 2024. Timu hiyo inatarajiwa kuondoka nchini mnamo Alhamisi.
Wachezaji waliripoti kambini Jumatano iliyopita na kuanza siku yao ya sita ya mazoezi Jumanne katika Hoteli ya Stadion jijini Nairobi.
Jumatatu, wachezaji 26 tu walikuwa wameripoti kambini kwa mazoezi.
Hata hivyo, wachezaji wanne Bridget Maria, kipa Velma Abwire, na mabeki Lorine Ilavonga na Rose Nangila kutoka Shule ya Wiyeta Girls, bado hawajaripoti kambini.
Akizungumza Jumatatu katika uwanja wa Kasarani Annex jijini Nairobi baada ya mazoezi, kocha wa Junior Starlets, Mildred Cheche, alionyesha imani yake katika maandalizi ya timu kwa mechi za kufuzu zijazo.
“Katika siku tano zilizopita, timu yetu imekuwa ikifanya mazoezi kwa bidii. Wachezaji wana hamu kubwa ya kushindana na ni vyema kutambua kwamba timu yetu inajumuisha wachezaji kutoka asili tofauti, timu, na shule. Hata hivyo, sina wasiwasi kuhusu tofauti hii, kwani wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika shughuli tofauti za mpira wa miguu,” alisema Cheche.
Cheche, ambaye ni kocha msaidizi wa Harambee Starlets na timu ya Ligi Kuu ya Taifa (NSL) ya Rainbow FC, alisisitiza umuhimu wa uzoefu uliopatikana kutokana na mashindano ya Talanta Hela, Chapa Dimba, na Michezo ya Shule.
“Kwa hiyo, tuna timu imara inayoweza kukabiliana na DRC vilivyo. Tuna imani katika uwezo wetu na tumejiandaa kabisa kuhakikisha tunapiga hatua kuingia raundi ya nne.”
Kenya itakuwa inashiriki kwenye mashindano haya kwa mara ya kwanza. Mlinzi Elizabeth Ochake, ambaye atawakilisha kwa mara ya kwanza, ameelezea azma ya timu kupigipania nchi yao.
“Tunapojiandaa hatuogopi yeyote. Tumefanya mazoezi kwa bidii chini ya uongozi wa benchi la ufundi na tuna imani katika uwezo wetu. Tunajua tutakutana na wapinzani wakali, lakini tumeazimia kujikakamua vilivyo. Tupo tayari,” alisema Ochake.
Timu tatu bora kutoka Shiriksho la Soka Barani Afrika (CAF), zitawakilisha Afrika katika Kombe la Dunia ambapo timu 16 kutoka mabara sita zitapambana katika jukwaa kubwa.
Kombe la Dunia litaandaliwa nchini Dominica kuanzia Oktoba 16, 2024, hadi Novemba 3, 2024.