Savula abaki motoni washtakiwa 13 wakiachiliwa
NA RICHARD MUNGUTI
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amewaondolea kesi washukiwa 13 walioshtakiwa pamoja na Naibu Gavana wa Kaunti ya Kakamega Ayub Savula katika kashfa ya kufyonza kutoka kwa serikali takriban Sh122 milioni.
Sasa Bw Savula, wake wake wawili–Melody Gatwiri Ringera na Hellen Jepkor Kemboi–na kampuni zao saba pamoja na washtakiwa wengine ambao ni watumishi wa serikali, wataendelea na kesi hii ya ufisadi wa Sh122,335,500.
Inadaiwa watumishi hao wa umma walimlipa kwa njia ya ufisadi Bw Savula, wake wake na kampuni za pesa hizo Sh122.3 milioni wakidai walikuwa na uwezo wa kutangaza masuala ya serikali katika magazeti na majarida yanayosomwa sana humu nchini.
Mashtaka yalisema Bw Savula, wake wake na kampuni zao, walijua hawakuwa na uwezo huo wa kutangaza huduma za serikali katika majarida.
Kesi hiyo ilipotajwa Jumanne, kiongozi wa mashtaka Bw Henry Kinyanjui alisema ameagizwa na DPP afutilie mbali kesi dhidi ya washtakiwa 13 lakini aendelee na kesi dhidi ya washtakiwa watakaosalia 15 akiwemo Bw Savula ambaye ni mbunge wa zamani wa Lugari.
Bw Kinyanjui aliomba hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bw Lucas Onyina atamatishe kesi dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari na Utangazaji Sammy Ishiundu Itemere.
Wengine walioachiliwa ni Edith Kainda Nkanata, Amos Matanga Tayari, Gladys Hadida Bwora, Gladys Isaka Mwanyika, Agren Jesca Ateka, Rachel Wanjiru Munge, Nellie Kibocha Nyachomba, Sammy Makau Mule, Martin Njoroge Njenga, Hannah Wangari Wanderi, Edmund Horrace Munene na Victor Owino Achola.
Watakaoendelea na kesi ni Bw Savula, Melody, Hellen na kampuni zao saba ambazo ni Sunday Publishers Limited, Melsav Company Limited, Johnnewton Communications, The Express Media Group, No Burns Protection Agencies Limited, Cross Continents Ventures Limited, na Shield Lock Limited.
Watumishi wa umma ambao hawakuondolewa kesi ni pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa kitengo cha utangazaji (GAA) Bw Dennis Kuko Chebitwey, Dickson Onala Nyandiga, Fredrick Okello Owiti, na Joseph Kamau Charagu.
Kuondolewa kwa mashtaka dhidi ya washtakiwa hao 13 kulifuatia kutathminiwa upya kwa ushahidi katika kashfa hiyo.
Wakati kesi hiyo imekuwa ikiendelea, washtakiwa wawili, Henry Mungasia Musambaga na Tabitha Nyaboke Oriba, waliaga dunia na kesi dhidi yao kutamatishwa.
“Baada ya kutathmini ushahidi uliopo dhidi ya washtakiwa 13, ni bayana hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kesi dhidi yao. Naomba mahakama ifutilie mbali kesi inayowakabili,” Bw Kinyanjui alimweleza Bw Onyina.
Wakili Ashitiva Mandale hakupinga ombi hilo dhidi ya washtakiwa hao 13 akisema “miaka sita imepita tangu wateja hawa wafikishwe kortini. Walipoteza kazi na mapato lakini hawapingi kesi dhidi yao ikizamishwa.”
Washtakiwa walikabiliwa na shtaka la kula njama kuilaghai serikali Sh122,335,500 kwa madai Bw Savula na makampuni yake yalikuwa na uwezo wa kutangaza miradi ya serikali.
Watumishi hao wa umma walishtakiwa kutumia mamlaka ya afisi zao vibaya kwa kuidhinisha makampuni saba ya Savula kulipwa Sh122,335,500 kinyume cha sheria.
Bw Savula pia ameshtakiwa kughushi barua ya kuidhinisha kampuni zake kutangaza masuala ya Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu na pia Wizara ya Ardhi.
Bw Savula, wake wake na kampuni zao, wanashtakiwa kujaribu kupokea kwa njia ya udanganyifu Sh119,000,000 kutoka kwa Wizara ya Utangazaji kati ya Julai 1, 2015, na Agosti 30, 2018.
Washtakiwa walikana mashtaka dhidi yao na wako nje kwa dhamana.