Viongozi wa ‘Mulembe’ watumia sukari kufufua upya nyota zao
NA MARY WANGARI
BAADHI ya wanasiasa na viongozi kutoka Magharibi mwa Kenya waliotemwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, wameangaziwa kwa kutumia masaibu yanayoandama sekta ya sukari nchini kama mbinu ya kufufua ndoto zao kisiasa.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula ameshutumu vikali kundi la wanasiasa anaodai wanatumia changamoto zinazoyumbisha viwanda vya sukari eneo hilo kujitafutia umaarufu kisiasa.
Amesema licha ya serikali kutenga mabilioni kwa lengo la kufadhili mikakati ya kufufua sekta ya sukari nchini, wapinzani wake kisiasa wamekuwa wakieneza porojo kuhusu njama za kuuza viwanda vinavyokabiliwa na wakati mgumu.
Huku akipuuzilia mbali madai ya kuwepo mipango ya kuuza Kiwanda cha Sukari cha Nzoia, Bw Wetangula alisema Bunge la Kitaifa limeidhinisha kiasi cha Sh1.7 bilioni kupitia Bajeti ya Ziada kwa lengo la kufufua sekta ya sukari nchini.
Kulingana na Spika Wetangula, fedha hizo zinajumuisha Sh300 milioni zilizotengewa Kampuni ya Sukari ya Nzoia ambapo Sh250 milioni zitatumika kulipa madeni yanayodaiwa na wakulima huku malimbikizi ya mishahara ya wafanyakazi yakilipwa kupitia Sh50 milioni.
Aliwasuta vikali badhi ya wanasiasa wa Magharibi akiwemo waziri wa zamani Eugene Wamalwa, aliyekuwa mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi na Mbunge wa sasa Kabuchai Majimbo Kalasinga, akidai wanatumia masaibu yanayokumba Kampuni ya Sukari ya Nzoia kwa sababu za kibinafsi.
“Viongozi wanaohubiri propaganda kwamba Nzoia imepangiwa kuuzwa ni manabii wa maangamizi. Katika muda wa wiki mbili zijazo Waziri wa Kilimo Mithika Linturi atazuru kampuni hiyo kuwasilisha fedha hizo. Itakuwa aibu kwa wanaoeneza uvumi,” alisema Spika Wetang’ula.
Amewataka wapinzani wake wakiongozwa na Mbunge wa Kabuchai, Majimbo Kalasinga, kukoma kuwapotosha wakulima kuhusu mipango ya serikali kwa viwanda vya sukari.
“Nataka kuwaeleza wanaotumia kampeni za Kampuni ya Sukari kufufua taaluma zao kisiasa kwamba hawatafaulu. Nzoia si bustani ya ufufuo.”
Kulingana na Bw Wetangula “habari njema ni kuwa Kiwanda cha Sukari cha Nzoia kimerejelea shughuli zake za kusaga sukari na wakulima wanalipwa pesa zao wiki mbili baada ya kuwasilisha miwa.”
Alisema kuwa wakulima, hasa kutoka eneo la Magharibi, wameteseka sana baada ya viwanda vya sukari kusambaratika akisema watapata afueni baada ya serikali kufufua kampuni hizo.