Makala

Serikali ya Lamu yaelimisha wageni maana ya ‘itabidi mzoee’

January 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imefaulisha juhudi za kupeana na kubandika majina ya sehemu mbalimbali za mji wa kale wa Lamu, ikiwemo vishoroba, vitongoji, mitaa, maeneo ya kupumzika ya umma na yale ya kuandaa mikutano na mabaraza.

Hatua hiyo imechukuliwa katika harakati za kuwasaidia wageni na watalii wanaozuru kisiwa cha Lamu kupata uelekezi sufufu, hivyo kuuzoea mji huo wa kihistoria.

Isitoshe, hatua hiyo itazuia wageni na watalii, hasa wale wanaozuru Lamu kwa mara ya kwanza dhidi ya kupotea wanapotembea kuingia ndani ya mji.

Kaunti pia imetumia nafasi hiyo kujitangaza kwani nembo rasmi ya Kaunti ya Lamu imewekwa katika kila kibandiko kilichotundikwa kwenye eneo husika.

Gavana wa Lamu Issa Timamy anasema hatua hiyo imechukuliwa kama njia mojawapo ya kuhakikisha kuna mpangilio bora wa mji wa kale ambao ni kivutio kikuu cha watalii wanaozuru kaunti hiyo.

“Lazima kuwe na mpangilio bora kwenye mji wetu wa kihistoria ili kuweza kuwavutia watalii kuzuru eneo hili. Na hii ndiyo sababu tukaafikia kuweka vibandiko vya majina katika kila sehemu. Vibandiko pia viko na maelezo ambayo yanawasaidia wale wanaoingia kisiwani Lamu kwa mara ya kwanza kujua wako wapi na ni wapi wanakofaa kwenda au kukaa kutekeleza shughuli gani,” akasema Bw Timamy.

Miongoni mwa maeneo yaliyobandikwa majina ya maelezo ni eneo la jeti kuu ya Lamu iliyoko karibu na mkahawa wa Mangrove.

Hapa, mja atapata bango maalum lenye majina ya sehemu zote kuu za mji wa kale wa Lamu, mji wenyewe uko eneobunge gani, ni kipi chafaa na kipi hakifai kamwe kufanywa kwenye mji wa kale wa Lamu miononi mwa maelezo mengine.

Ni kupitia vibandiko hivyo vyenye nembo ya kaunti ya Lamu ambapo pia kwa anayewasili Lamu atatambua kuwepo kwa jeti mbili ambazo watu hushuka kutoka kwa boti na mashua kuingia kisiwani.

Jeti hizo zinajumuisha ile ya ‘Zamani’ iliyoko mbele ya ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (KPA), na ‘Jeti Mpya’ ipatikanayo mbele ya mkahawa wa Mangrove mjini Lamu.

Kaunti pia iliweka vibandiko kwenye eneo la mikutano au bustani ya ‘Mkunguni’ pia wakiita ‘Forodhani’.

Kibandiko kwenye eneo la mikutano au bustani ya ‘Mkunguni’, sehemu ambayo pia huitwa ‘Forodhani’. PICHA | KALUME KAZUNGU

Sehemu ya mapumziko ya mbele ya Hospitali Kuu ya Kaunti ya King Fahd na kwenye lango kuu la kuingilia hospitalini humo pia ziliwekwa vibandiko na maelekezo ya ni wapi pa kwenda kuepuka kukorogeka.

Kaunti vile vile imehakikisha sehemu mbalimbali za eneo la mbele ya mji wa kale wa Lamu ambayo ni mkabala na ufuo wa bahari zinabandikwa majina, maelekezo na hata maonyo kwa wote wanaokaa au kutembelea kisiwa cha Lamu.

Utapata kuna eneo maalum lililotengwa na kubandikwa maelezo ya kuwa sehemu ya vyakula, maeneo ya kubarizi na kadhalika.

Baadhi ya wenyeji, wageni na watalii waliohojiwa na Taifa Leo Jumatano waliusifu mpangilio huo waliodai umewaepushia zahama za kuchanganyikiwa kwenye matembezi au kuzurura kwao kwa kila siku mjini.

Bw Ahmed Hussein anasema kwa miaka mingi wamekuwa wakiililia na kuisukuma kaunti kuibuka na mpango huo wa kupeana majina miji, mitaa, vitongoji na vishoroba vya mji wa Lamu.

Anasema ni kupitia mpango huo ambapo sera za mji huo wa kale ambao ni ngome kuu ya watalii zitauzwa vyema.

“Watalii wakifika kisiwani hupata maarifa ya ni eneo gani watembelee kwani vibandiko huwawezesha kujua hili ni jumba la makavazi ya Lamu, lile ni jumba la Lamu Fort, ule ni msikiti wa zamani na wa kihistoria na kadhalika,” akasema Bw Hussein.

Bi Firdaus Alwy anasema maonyo na jumbe zilizoko kwenye baadhi ya vibandiko pia zimesaidia kuwaelimisha wote wanaoishi Lamu, iwe ni wenyeji, wageni na watalii.

“Kwa mfano, kwenye jeti ya mangrove ambayo ndiyo lango kuu la kuingilia kisiwani Lamu, utapata bango na vibandiko vinavyowatahadarisha wanaoingia mjini kuhusu mtindo wa mavazi unaokubalika, tabia zikubalikazo mjini na kadhalika. Yaani anayeingia mjini hana sababu za kukaidi itikadi na mila kwani huonywa mapema,” akasema Bi Alwy.

Omar Harun anasema majina ya sehemu mbalimbali yaliyobandikwa kisiwani Lamu ni suluhisho tosha la waja kuuzoea mji wapende wasipende.

Mnamo 2001, Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) liliuorodhesha mji wa kale wa Lamu kuwa miongoni mwa maeneo yanayotambuliwa zaidi duniani kwa kuhifadhi ukale wake-yaani Unesco World Heritage site.

Miongoni mwa vigezo vilivyotumika na Unesco kuuteua mji wa kale wa Lamu ni jinsi wenyeji walivyofaulu kuenzi tamaduni zao, ikiwemo kutembea kwa miguu, punda na mikokoteni, ikizingatiwa kuwa vibarabara vilivyoko mjini ni vyembamba na vinavyokosa uwezo wa kupitisha magari, baiskeli au pikipiki.

Kituo cha kutunza punda. PICHA | KALUME KAZUNGU