Habari za Kitaifa

Jela yapanda vigingi kurejesha ardhi iliyonyakuliwa

February 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA EVANS JAOLA

SERIKALI imeanza kuweka vigingi kwenye ardhi iliyonyakuliwa ya Magereza Kitale, wiki chache tu baada ya Rais William Ruto kuagiza kurejeshwa kwa ekari 2,700 ambazo zilinyakuliwa na watu binafsi kinyume cha sheria.

Kikosi cha pamoja cha usalama kiliwasili Jumatano katika eneo hilo ndani ya magari 10, kikiwa na zana za kutuliza ghasia.

Vikosi vya usalama vinavyojumuisha Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Upelelezi wa Jinai DCI, na maafisa wa Wizara ya Ardhi walisimamia zoezi hilo lililoongozwa na Naibu Kamishna wa Magereza Charles Mutembei, huku wafungwa wakisaidia kusimamisha minara.

Kigingi cha simiti chenye maandiko ya kuthibitisha shamba ni la idara ya mahakama. PICHA | EVANS JAOLA

Polisi hao waliokuwa waliwakamata wakazi huku maafisa hao wakiwa kimya wakitekeleza zoezi hilo chini ya uongozi wa afisa mkuu wa serikali aliyekuwa na ramani ya serikali.

Katika ziara yake Kaunti ya Trans Nzoia mnamo Januari 16, 2024, Rais Ruto alitoa onyo kali kwa wale walionyakua ardhi ya gereza la Kitale kuondoka la sivyo wafurushwe na kushtakiwa.

Agizo la Rais lilizua mvutano katika kaunti hiyo, ambapo wanyakuzi wa ardhi wanasemekana kuwa watu wenye ushawishi.
Baadhi ya maeneo ambayo maafisa hao waliweka vigingi ni pamoja na Wamuini, Kephis, Maili Tatu, Top Station Primary, Mitambo, na eneo la Gereza la Annex.

Maafisa wa magereza wasimamia wafungwa wakipanda vigingi katika shamba la Kephis ambalo linamilikiwa na Idara ya Magereza mnamo Januari 31, 2024. Shughuli hiyo iliongozwa na Naibu Kamishna wa Magereza Charles Mutembei. PICHA | EVANS JAOLA

Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Kaunti Ndogo ya Kitale Magharibi, Patrick Gaitarira na mwenzake wa Kwanza, James Odera walijumuika na maafisa wengine katika operesheni hiyo.

Maafisa hao wenye silaha waliendesha zoezi hilo bila pingamizi kutoka kwa walengwa wa ardhi husika.

Mkuu wa Polisi Trans Nzoia Magharibi Patrick Gaitirira aangalia ramani kuthibitisha mipaka ya ardhi ya magereza. PICHA | EVANS JAOLA

Uwepo mkubwa wa maafisa hao ulisimamisha biashara katika maeneo ya Village Inn, Mitambo, na Wamuini huku kukiwa na hofu kutoka kwa wakazi.

Bw Mutembei alikataa kuzungumzia zoezi hilo akisema wanatekeleza tu maagizo ya serikali.

“Kwa sasa siwezi kuzungumzia chochote. Tunatekeleza tu maagizo ya serikali,” afisa mwingine wa magereza aliambia waandishi wakati wa zoezi hilo.