Makala

Polisi avuta bangi ‘cha lazima’

February 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

POLISI mmoja amelazwa katika Hospitali Kuu ya Murang’a akiwa hajielewi baada ya kushurutishwa na genge mtaani kuvuta misokoto miwili ya bangi.

Polisi huyo alikuwa pamoja na wengine wawili waliofika katika mtaa wa Kayole kuandama mtandao wa walanguzi wa mihadarati.

Inadaiwa genge hilo liliwaambia waziwazi kuwa katika kipindi cha chini ya nusu saa, kulikuwa na maafisa wengine waliokuwa wamechukua hongo kuruhusu biashara haramu ya bangi kuendelea.

“Genge hilo lilidai kwamba hata dakika 20 hazikuwa zimepita tangu polisi wengine wafike hapo na kuchukua hongo,” akasema mhudumu wa bodaboda aliyeshuhudia kisa hicho.

Alisema mabishano ya wanachama wa genge hilo na polisi yaligeuka kuwa mabaya.

Inadaiwa maafisa wawili walifanikiwa kujiondoa katika eneo la tukio lakini mmoja huyo aliandamwa na kushurutishwa avute bangi kwa lazima.

Ripoti ambayo kituo cha polisi cha Murang’a kiliandaa kuhusu kisa hicho ilisema afisa huyo alishambuliwa na watu ambao hawajulikani.

“Tulipata ripoti kwamba kulikuwa na makabiliano kati ya vijana katika kundi mojawapo mtaani na polisi waliokuwa wamevalia kiraia,” ikasema ripoti ya polisi.

Iliongeza kwamba maafisa walitumwa eneo hilo na ndipo “mwanamume aliyetambuliwa kuwa ni polisi wa cheo cha konstebo alipatikana akiwa amepoteza fahamu walioshuhudia wakisema kwamba alishurutishwa kuvuta kinachoaminika ni bangi”.

Afisa huyo alikimbizwa katika hospitali ambapo kwa sasa amelazwa akitibiwa athari za kuzimia chini ya shinikizo za ulevi kupindukia.

Kamanda wa Polisi Murang’a Mashariki Mary Wakuu alisema kisa hicho kinachunguzwa na msako utafanywa kunasa washukiwa.

Bi Wakuu alisema mtaa huo wa Kayole kwa muda umekuwa katika darubini ya maafisa wa usalama kutokana na ulanguzi wa mihadarati.

“Ni mtaa ambao lazima tutausafisha. Pia natoa onyo kwa polisi wawe wa kutekeleza busara na uadilifu kazini. Hayo mambo yote yatachunguzwa na taswira kamili itaandaliwa ripoti,” akasema Bi Wakuu.

Alisema watachunguza ikiwa polisi hao watatu nao walikuwa wakiitisha hongo jinsi ilivyodaiwa.

[email protected]