JSC yaombwa imtimue kazini Jaji Mkuu Koome
NA RICHARD MUNGUTI
OMBI la kumtimua kazini Jaji Mkuu (CJ) Martha Koome limewasilishwa mahakamani na mkazi wa Homa Bay kwa madai alitumia mamlaka yake vibaya wakati wa uteuzi wa jopo la kutatua mizozo ya kodi.
Kesi hii iliyowasilishwa na Bw Michael Kojo Oloo imezidisha joto na vuta nikuvute katika ofisi ya Jaji Mkuu ambaye amezongwa na cheche za wanasiasa kutokana na maamuzi yanayokinzana na mwongozo wa serikali ya Kenya Kwanza kuhusu miradi mbalimbali.
Katika siku za hivi punde, Jaji Koome na Rais William Ruto wamelumbana hadharani kutokana na kubatilishwa kwa sheria ya kodi ya nyumba.
Katika kesi hii iliyowasilishwa na Bw Otieno, Jaji Mkuu amelaumiwa kwa kuwateua wanachama 22 wa bodi ya kusuluhisha mizozo ya kodi.
“Jaji Koome ameongeza wanachama wawili katika bodi hiyo inayofaa kuwa na wanachama 20 na kuwalimbikizia wananchi mzigo wa kodi,” akasema Bw Otieno katika ombi lake.
Ombi hilo la kumtimua Koome kazini lilipokewa katika ofisi za tume ya kuwaajiri watumishi wa idara ya mahakama JSC na kupigwa stampu mnamo Januari 31, 2024.
Wanachama ambao waliteuliwa na Jaji Koome kujiunga na bodi hiyo ya kutatua mizozo ya kodi (TAT) na kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali ni Elisha Njeru, Kadzo Ngala Delilah, Cheluget Edwin Kiprono, Tanvir Ali Mohsin, Mutuma Robert Mugambi na Karingo Jephthah Njagi.
Wanachama wengine wa TAT ni Mukuha Grace Gathoni, Oluoch Rodney Odhiambo, Kibet Abraham Kiprotich, Mayaka Cynthia Boundi, Ogaga Gloria Awuor, Ongeri Walter Juma, Olochike Sankale Spencer, Diriye Abdullahi Mohamed, Vikiru Timothy Bunyali.
Pia Kamolo Erick Onyango , Kashindi George Ashiono,Ng’ang’a Eunice Njeri, Muga Christine Anyango, Terer Boniface Kibiy, Makau Martin Mutiso James na Bernadette Muthira Gitari waliteuliwa kuwa wanachama wa TAT.
Katika kesi ya kumng’atua mamlakani Jaji Koome Bw Otieno inasema wanachama wa TAT hawapasi kuwa chini ya watu 15 na hawapasi kuwa zaidi ya 20.
“Jaji Koome aliteua wanachama 22 kinyume cha sheria na kutumia mamlaka yake vibaya,” asema Bw Otieno.
Anasema JSC iko na mamlaka na uwezo wa kumng’atua mamlakani Jaji Koome kwa vile alikaidi sheria na utovu wa nidhamu.
Mlalamishi huyu anasena Sheria nambari 5(1) zinazowadhibiti watumishi wa umma inasema kuwa matendo ya Jaji aidha katika safu ya umma ama faraghani anafaa kutenda mambo yanayoonyesha ametenda haki na kuhudumia umma ipasavyo.
Mlalamishi anasema vitendo vya Jaji havifai kuletea umma aibu kwa namna yoyote ile.
Bw Otieno anaomba JSC ikubali ombi lake na impendekezee Rais Ruto ateue jopo la kumchunguza Jaji Koome kwa lengo la kumwachisha kazi.