Habari za Kitaifa

Gesi ilianza kuvuja mapema kabla mlipuko ulioua na kujeruhi wengi Embakasi

February 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA DANIEL OGETTA

KIJIJI cha Miradi, eneo la Embakasi Nairobi kiliamkia kisa cha kutisha cha nyumba na makazi kuchomeka yakabaki majivu, maisha kubadilika kabisa na jinsi yalivyokuwa Alhamisi jioni jua lilipozama.

Kijiji hicho cha wakazi wa pato la chini kilicho katikati ya Mtaa wa Nyayo na kampuni kadhaa, kilikuwa kimebaki mahame kufuatia mkasa wa mlipuko wa gesi.

Katika majira ya asubuhi, kulingana na mkazi Bi Vanessa Okeyo, alihesabu miili iliyotapakaa sakafuni.

Wengine walikuwa na majeraha ya kutisha ya moto na walikuwa hawawezi kutembea.

Alhamisi iliyoisha vizuri siku iliyotangulia kumbe ilikuwa ipishe Ijumaa ya kushtua: nguo zilizotapakaa kote, magari yaliyochomeka na rundo la mali iliyoteketea kuashiria janga lililotokea usiku huo.

Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura aliyefika mwendo wa saa tano asubuhi alitaja mkasa huo kuwa wa kushtua.

Soma pia Wawili wathibitishwa kufariki, mamia wakijeruhiwa katika mlipuko wa gesi Embakasi

Jinsi kituo hicho cha gesi kilivyojengwa karibu na makazi kunaibua maswali mengi haswa baada ya Idara ya Udhibiti wa Kawi kufichua kwamba kampuni hiyo haikuwa na leseni ya kuweka biashara ya gesi eneo hilo.

Wakazi kwa miaka mingi walilalamikia kuhusu usalama wa kuweka kituo hicho cha gesi karibu nao.

Sasa imebainika kwamba ilikuwa suala la lini mkasa ungetokea, sio iwapo ungetokea. Lakini iwapo mwenye kituo hicho angesikiza kilio cha wakazi, labda mkasa huo ungeepukika, kulingana na simulizi za walioshuhudia.

Kutoka saa tatu usiku, wenye biashara na wenye maduka walimpigia simu mwenye gereji kumwambia kwamba kulikuwa na sauti iliyoaminika kuwa ya gesi iliyokuwa inavuja kutoka kwa mojawapo ya malori yaliyokuwa yameegeshwa humo.

Kufikia saa nne usiku, harufu kali ya gesi tayari ilikuwa imeshazagaa kote.

Kila sekunde iliyopita, walijua janga lilikuwa linanukia.

Kupiga simu kwa nambari ya dharura ya polisi 999 hakukuzaa matunda, kulingana na waliokuwepo.

“Walinipigia simu baadaye baada ya mlipuko kutokea. Niliwaambia mkasa tayari ushafanyika.”

Haijabainika wazi saa ambapo gesi ililipuka, wengi wanasema ilitokea saa tano unusu usiku, wengine wakisema ilikuwa usiku wa manane. Hata hivyo, wengi wanakubaliana kwamba ilihisi kama jehanamu.

Mlipuko mkubwa ulisikika, kisha tonge kubwa la moto likazagaa mtaani kote.

Wengi wanasema walihisi wakiwa kama wako kwenye filamu ya kutisha, ila kwa hili, kila kitu kilikuwa kweli.