Ajuza Rael Mayaka katika kesi ya kung’oa mtoto macho aachiliwa huru
RUTH MBULA NA WYCLIFFE NYABERI
MAHAKAMA ya Rufaa mjini Kisii Ijumaa ilimwachilia huru Rael Mayaka, 80, ambaye alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kumng’oa macho mjukuu wake, Junior Sagini.
Jaji Kiarie Waweru akimwachilia Mayaka alisema upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi hiyo kwa viwango visivyoweza kutiliwa shaka.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Kiarie alisema hakuna ushahidi unaoonyesha nyanya Rael alitenda kosa kama alivyoshtakiwa.
“Hakukuwa na ushahidi wa kuunga mkono shtaka la madhara makubwa. Afisa wa uchunguzi hakutoa ushahidi ikiwa alichunguza ushahidi kwa madhara makubwa. Hukumu hiyo imetengwa,” alisema Jaji Kiarie.
Soma pia: Mtoto Sagini: Washtakiwa waliomng’oa macho wasukumwa jela miaka 40, 10 na 5
Bi Mayaka alijawa na furaha nje ya mahakama na alianza kuimba na kucheza huku akimshukuru Mungu kwa kupata uhuru wake.
“Asante asante. Mungu anasaidia. Huyu Mungu amesaidia. Na yule mtoto, ni mzuri,” ajuza huyo alisema huku akimpiga pambaja wakili wake, Kerosi Ondieki kwa furaha.
Aliongeza, “Nimetoka, Mungu amenisaidia…. Ninaenda nyumbani kwangu. Hakuna kitu, niko peke yangu nyumbani kwangu, hakuna mtoto, mjukuu wangu hayupo. Nilikuwa gerezani, asante Mungu.”
Bi Mayaka alifungwa jela pamoja na bintiye Pacificah Nyakerario na mjukuu mwingine Alex Maina Ochogo mnamo Juni 2023.
Ochogo (binamu ya Sagini), Nyakerario (shangazi ya Sagini) na Mayaka (nyanyake Sagini) walihukumiwa kifungo cha miaka 40, 10 na mitano mtawalia, kwa kumng’oa macho mtoto huyo wa miaka mitatu kwa wakati huo.
Ochogo na Nyakerario hawakukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Wakili wa Mayaka, Bw Kerosi alisema kwamba mlalamishi hatimaye amepatikana hana hatia ingawa alishtakiwa kimakosa.
“Tangu mwanzo, niliamini kuwa Bi Mayaka hakuwa na hatia. Alikuwa mlezi wa mtoto. Yeye ndiye aliyekuwa akimtunza Sagini. Yeye ndiye aliyekuwa akitafuta mtu wa kurithi mali yake. Kwa hivyo hakuwa na sababu ya kumdhuru,” akasema Bw Kerosi baada ya mteja wake kuachiliwa.
Aliongeza, “Tatizo ambalo nimekumbana nalo na ninachowaomba wananchi kwa ujumla ni kwamba tusiwashtumu watu bali tusubiri mahakama na vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yao na kuleta matokeo. Wananchi wawe na subira kila mtu anapokamatwa. Mwacheni Mayaka aishi maisha yake, yuko katika siku zake za machweo na bora aachwe aishi muda uliobaki kwa amani maana amepitia changamoto kubwa.”
Soma pia: Mtoto Junior Sagini na dadake kupata matunzo spesheli kutoka kwa serikali
Hakimu Mkazi Mwandamizi Christine Ogweno alipokuwa akiwahukumu watatu hao, alisema alizingatia umri wao, huku Nyakerario na Mayaka wakiwa na miaka 51 na 80 mtawalia. Mahakama haikuwa na uhakika ikiwa Ochogo alikuwa na umri wa miaka 27 au 37.
“Mahakama inazingatia jukumu lililotekelezwa haswa na kila mmoja wa wahalifu watatu. Mtoto huyo alipoteza macho yake mikononi mwa binamu yake, Alex Maina Ochogo,” akasema Bi Ogweno.
Hakimu Ogweno alisema Nyakerario na Mayaka walikuwa wasaidizi wa kufanya uhalifu na kwamba jukumu lao finyu katika kutenda kosa lilizingatiwa.
“Mtazamo wa jumuiya na ripoti ya kabla ya hukumu inasalia kuwa mbaya kwa Nyakerario. Kesi ni tofauti kwa Mayaka ambaye aliwatunza mwathiriwa na dadake huku mama yao akihangaika kujikimu mbali na nyumbani kwao,” akasema Bi Ogweno alipokuwa akiwahukumu wanawake hao wawili.
Kabla ya Desemba 13, 2022, Hakimu alisema, mtoto huyo aliishi maisha ya kawaida na yaliyotarajiwa chini ya uangalizi wa nyanya yake, Bi Mayaka.
Hata hivyo, Bi Ogweno alisema, matukio ya Desemba 13, 2022, yatakumbukwa milele katika akili ya Sagini na kuchorwa kwenye kumbukizi za maisha yake kwani alipoteza macho na kuwa kipofu.
Sagini alivamiwa mnamo Desemba 13, 2022, nyumbani kwao Ikuruma katika kaunti ndogo ya Marani.
Mahakama ya chini ilithibitisha kwamba macho ya mvulana huyo mdogo yalitolewa na binamu yake, Ochogo, kwa kutumia kisu chenye ncha kali, moja baada ya jingine.