Nigeria pazuri kuzoa taji la nne la Afcon baada ya kudengua Angola katika robo-fainali
Na MASHIRIKA
WAFALME mara tatu wa Kombe la Afrika (Afcon), Nigeria, ndio walikuwa wa kwanza kufuzu kwa nusu-fainali baada ya kupepeta Angola 1-0 ugani Felix Houphouet Boigny jijini Abidjan mnamo Ijumaa.
Bao la pekee katika pambano hilo la Ijumaa lilipachikwa wavuni na fowadi Ademola Lookman anayepiga soka ya kulipwa nchini Italia akivalia jezi za Atalanta katika Serie A.
Lookman, 26, sasa anajivunia mabao matatu kapuni na ni miongoni mwa masogora wanaopigiwa upatu wa kuibuka wafungaji bora kwenye makala ya 34 ya Afcon 2023.
Nigeria sasa wametinga nusu-fainali za Afcon mara 15 kutokana na makala 18 yaliyopita ya kipute hicho.
Walianza safari yao ya mwaka huu kwa kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Equatorial Guinea katika Kundi A kabla ya kupepeta wenyeji Cote d’Ivoire 1-0 na kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Guinea-Bissau.
Walidengua Cameroon kwenye hatua ya 16-bora kwa mabao 2-0.
Angola kwa upande wao waliibuka washindi wa Kundi D kwa alama saba baada ya kuwapiga kumbo Burkina Faso (2-0), Mauritania (3-2) na kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Algeria waliotawazwa mabingwa wa Afcon 2019.
Kikosi hicho kinachoshikilia nafasi ya 117 duniani kilikomoa Namibia 3-0 katika hatua ya 16-bora na kitaendelea kusubiri zaidi kutinga raundi ya nne-bora katika historia ya Afcon.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO