• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wakili wa Miguna kizimbani  kwa dai alihepa ‘vuta pumzi’

Wakili wa Miguna kizimbani kwa dai alihepa ‘vuta pumzi’

Wakili Aaron Ndubi aliyemwakilisha Dkt Miguna Miguna. Alitiwa nguvuni Februari 9 usiku mwendo wa saa mbili na nusu akielekea nyumbani katika barabara ya Jakaya Kikwete jijini Nairobi. Picha/ Maktaba

Na RICHARD MUNGUTI 

Kwa Muhtasari:

  • Bw Ndubi alitiwa nguvuni Ijumaa usiku mwendo wa saa mbili na nusu akielekea nyumbani katika barabara ya Jakaya Kikwete
  • Alikaidi agizo la afisa wa polisi kumtaka apulize kifaa cha kuwatambua madereva walevi almaarufu ‘vuta pumzi’
  • Mawakili 20 walifika mbele ya Hakimu Riany kumwakilisha mshtakiwa huyo
  • Pia alikabiliwa na shtaka la kuyazuia magari mengine kwenye barabara hiyo

MMOJA wa mawakili 15 waliokuwa wanamtetea mwanaharakati na wakili mwenye tajriba kuu Dkt Miguna Miguna aliyefurushwa nchini kinyume cha maagizo ya Mahakama Kuu alishtakiwa Jumatatu kwa kukataa kupuliza kifaa cha kuwatambua madereva walevi.

Bw Aaron Ndubi aliyefikishwa mbele ya hakimu mkazi katika mahakama ya Milimani, Bi Elector Riany na kukanusha mashtaka mawili dhidi yake alikuwa mstari wa mbele kukashifu maafisa wa polisi waliokaidi agizo la Jaji Luka Kimaru kumfikisha Dkt Miguna katika mahakama Kuu.

Kutokana na kutiwa nguvuni kwa Bw Ndubi, mawakili 20 walifika mbele ya Bi Riany kumwakilisha mshtakiwa huyo.

Wakiongozwa na wakili Dkt John Khaminwa, mawakili hao walidai kuwa hakuna shtaka halisi lililokuwa mbele ya mahakama lenye mashiko ya kisheria.

“Wakati ukiwadia tutaithibitishia hii mahakama kwamba hakuna shtaka halisi liliwasilishwa dhidi ya afisa huyu wa hii mahakama,” Dkt Khaminwa alimweleza hakimu.

 

Siku tatu ndani

Alisema kwamba wakili Ndubi alitiwa nguvuni Ijumaa usiku mwendo wa saa mbili na nusu akielekea nyumbani katika barabara ya Jakaya Kikwete na kuzuiliwa katika korokoro ya polisi hadi Jumatatu alipofikishwa kortini.

“Naomba hii mahakama imwachilie mshtakiwa ambaye ni wakili mwenye tajriba ya juu kwa dhamana,” alirai Dkt Khaminwa.

Bi Riany alifahamishwa kuwa mshtakiwa ni wakili wa mahakama na “anaelewa na kujua anachopaswa kufanya kama mtaalamu wa masuala ya sheria.”

Mahakama iliombwa pia iamuru mshtakiwa apewe nakala za mashahidi aandae utetezi wake.

“Naomba hii mahakama iamuru tupewe ushahidi wote pamoja na nakala za taarifa walizoandikisha mashahidi,” Dkt Khaminwa alimsihi hakimu aagize upande wa mashtaka.

 

Kukaidi agizo

Ombi hilo la halikupingwa na kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu kwamba atampa Dkt Khaminwa nakala zote za mashahidi na taarifa zitakazotegemewa kwa ushahidi wa kuthibitisha kwamba Bw Ndubi alikaidi agizo la afisa wa polisi kumtaka apulize kifaa cha kuwatambua madereva walevi.

Bw Riany alikubali ombi la mshtakiwa na kuamuru alipe dhamana ya pesa tasilimu ya Sh30,000. Pia aliamuru apewe nakala zote za ushahidi aandae utetezi wake.

Mashtaka dhidi ya Bw Ndubi ni kwamba alikataa agizo la afisa wa polisi akiwa amevalia sare rasmi ya kazi alipotakiwa kupuliza kifaa cha kuwatambua walevi.

Pia alikabiliwa na shtaka la kuyazuia magari mengine kwenye barabara hiyo ya Jakaya Kikwete mnamo Feburuari 11, 2018. Kesi imeorodheshwa kusikizwa Feburuari 23.

 

You can share this post!

Wanawake watengewa nafasi 160 pekee kwenye jeshi

Ashtuka mke kukubali ajiburudishe na kahaba

adminleo