Makala

Mwanamume wa nywele za rasta adai mfumo wa Mungu ni ‘up-bottom’

February 4th, 2024 2 min read

NA RICHARD MAOSI

MKAZI mmoja wa Maela, Kaunti ndogo ya Naivasha ameshangaza wengi kwa kutangaza rasmi kwamba ana upako na ametumwa na Mungu kuokoa dunia.

Bw Warren Maloba ambaye ana mtindo wa nywele za rasta anasema mkesha wa kuamkia Krismasi mwaka 2023, Mungu alimpa ‘ufunuo’ akaupeleke kwa wanadamu kote duniani.

Ni kampeni ambayo ameamua itaanzia Kenya kabla ya kupenya na kufikia mataifa mengine duniani.

“Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha watu wake na ameona mahangaiko ambayo mwananchi wa kawaida anapitia,” asema Bw Maloba.

Akisimulia matukio ya usiku huo wa Desemba 24, 2023, Bw Maloba anasema alikuwa nyumbani kwake akipumzika aliposhtukia akiitwa jina lake lote kwa sauti kubwa.

Siku iliyotangulia, alikuwa amefunga kutwa nzima bila kula chochote akitarajia kuona miujiza.

Kwanza, anaeleza alipata maono na hatimaye “nikapatiwa ufunguo wa kuingia mbinguni”.

Aidha anasema katika dunia ya sasa, watu wanastahili kumjua Mungu ni nani.

Isitoshe anasema mfumo wa Mwenyezi Mungu ni ‘Up-Bottom’.

Pia anadai kunafaa kuwa na tofauti kati ya shetani, ibilisi, na mpinga Yesu Kristo.

Anaambia Taifa Jumapili kwamba mifumo ya kiuchumi inayopendekezwa na mataifa mengi haina tija yoyote na ndiposa binadamu katika mataifa mengi wanaendelea kutaabika “na bado wataendelea kuteseka”.

“Ukiangalia hali ya maisha ya sasa, mtu akijaribu kuinuka anakandamizwa na matajiri. Hii inaashiria kwamba maskini ataendelea kuwa maskini,” asema.

Anatoa mfano ambapo baadhi ya watu wanapokea mishahara mikubwa ilhali maskini wanaendelea kupokonywa kile kidogo walicho nacho.

Anasema makato ya juu kwa mishahara na mapata ya mahasla huleta vilio kwa wanyonge.

Vilevile anadai vijana wengi wasiokuwa na hatia wamesukumwa gerezani hata bila hatia kwa sababu hawana hela za kufanikisha upatikanaji wa haki.

“Hivi karibuni Mungu ameamua kwamba atachukua usukani wa dunia nzima na ataweka utawala wake katika mataifa yaliyoyumba,” asema.

Kulingana na Bw Maloba, hivi sasa ameanza kutekeleza kazi ambayo ameitiwa na atatumia kila mbinu kuhakikisha ujumbe unafika katika kila sehemu ya dunia.

Bw Maloba anasema Mungu “ananitumia kama chombo kukomboa hii dunia ambayo imejaa manyanyaso.”

Bw Warren Maloba ambaye ni mkazi wa Maela eneo la Naivasha katika Kaunti ya Nakuru ambaye alidai kuwa Mungu kampa ujumbe wa kuwapa raia kuhusu hali ya maisha na mambo mengine kwa ujumla. PICHA | RICHARD MAOSI