Ukiwa Mombasa, huhitaji kula nyumbani, barabarani pekee unashiba!
NA FATUMA BUGU
UTAMADUNI wa kula aina mbalimbali ya vyakula vya asili ya Pwani mitaani unazidi kufana katika Kaunti ya Mombasa, huku aina ya mapishi ambayo miaka iliyopita yangepatikana tu hotelini sasa yakipakuliwa kandokando ya barabara.
Hali hii imewachochea vijana kujitosa katika biashara hiyo, wakazi wakichangamkia mtindo huo wa kununua mapochopocho njiani, ambao umenoga katika jiji la Mombasa.
Ulaji wa vyakula vyenye asili ya Pwani jijini Mombasa ni miongoni mwa tamaduni zinazoenziwa sana na wenyeji wa eneo hilo.
Bila shaka wageni wanapozuru eneo hilo, mapochopocho kama viazi karai, bajia, kachiri za mihogo, achari na mishikaki ni baadhi tu ya milo ambayo huenda ikawaacha wengi wakidondokwa na mate mdomoni.
Katika miaka ya awali vyakula hivyo vilikuwa vikipikwa sana mitaani tu na kuuzwa baina ya wenyeji vitongojini.
Akina mama walitumia ujuzi wa kuandaa vyakula hivyo kama njia ya kujisakia tonge. Licha ya hayo, mtindo unabadilika vyakula hivi na vingine vingi vikipikwa kila pembe ya jiji la Mombasa.
Ajuza ambaye ameishi katika eneo la Mvita kwa zaidi ya miaka 30 Bi Grace Kavodha, anasema jikoni kulikuwa kwa kina mama pekee ila sasa hata vijana wa kiume wamejitosa kupika na kuuza chakula hicho.
“Zamani kina mama walikuwa wakipika viazi wanaviuza majumbani kama mila na desturi na hata shuleni kuwauzia wanafunzi. Lakini sasa vyakula hivi unavipata kila mahali kwanza jioni jijini ni kama mchana,” alisema Bi Kavodha.
Shawarma, bajia, katilesi, tikka, mkate wa mayai na viazi karai ni vyakula ambavyo vimetia fora katika mitaa mingi, mitaa ikisheheni harufu tamu ya mapochopocho hayo kila kona.
“Baadhi ya hivi vyakula tulikuwa tunavisikia tu au kuviona kwenye runinga kwa kuwa hoteli nazo zilikuwa hazishikiki kwa kuwa zilikuwa ghali, kwanza shawarma, lakini sasa ni kama samaki, anapatikana kote baharini,” aliongeza Bi Kavodha.
Hali hiyo imewashinikiza wengi kuanza utamaduni wa kula mitaani, wakidai kuwa huo ndio mtindo wa kisasa unaowapa uhuru wa kujichagulia watakacho.
Mwendeshaji tuktuk katika jiji la Mombasa Bw Daniel Makali, anasema wakati mwengine hasa kwa sababu ya jua kali la Mombasa, yeye hupendelea kula nje akibarizi na kupunga upepo wa bahari.
“Si kila siku tunapika nyumbani, wakati mwengine tunatoka kula nje maana hata chapati na maharagwe yaliokolea nazi utayapata mitaani kisha unateremsha na sharubati ya ukwaju au miwa. Maisha yamekuwa raha,” anasema Bw Makali.
Ni mwamko mpya wa tamaduni za kipwani, vijana wakijitosa katika upishi wa vyakula hivyo hasa kutokana na maakuli hayo kupata umaarufu.
“Wateja wako wengi sana kuanzia wanafunzi hadi wale wanaotoka kazini hupenda sana kula viazi, sambusa na makachiri, wanazipenda sana,” anasema Bw Rogers Paul,19, ambaye huuza viazi vya kukaanga kujichumia riziki.
Wauzaji wa vyakula hivyo wanaeleza kuwa kuwepo kwa masoko ya Markiti na Mwembe Tayari kunachochea biashara hiyo kwani watu wanapofanya ununuzi, wao hujipatia milo hiyo wanapotaka kujipumzisha kabla ya kuendelea na shughuli.
Maeneo maarufu ambayo huuza vyakula hivyo ni kama Kizingo, Majengo, Tudor na hata katika mitaa mbalimbali kama vile Bamburi, Spaki, Saba Saba na kwingineko.
Licha ya hayo yote, huenda serikali ya kaunti na asasi nyingine muhimu zikahitajika kuingilia kati ili kuhakikisha kuwa biashara zinazoshamiri zinafuata kanuni hasa kwa usalama na afya ya umma.
Kulingana na Sheria ya Chakula na Dawa, Sura ya 254, hakuna chakula kinachopaswa kuuzwa kando ya barabara nchini.
Hata hivyo, ikizingatiwa kuwa kaunti ya Mombasa ina utamaduni wa uuzaji wa chakula mitaani uliokita mizizi, serikali ya kaunti ya Mombasa iko mbioni kuingilia kati ili kudhibiti biashara hizo.
Kulingana na afisa mkuu wa afya ya umma wa Mombasa, Bw Abdallah Daleno, kaunti inatayarisha sera mpya ya usalama wa chakula ambayo itasimamia biashara hizo.
“Hii bado haijaidhinishwa, bado iko katika muundo wa rasimu. Kwa sasa hakuna wauzaji wa chakula mitaani walioidhinishwa kufanya kazi, hakuna leseni zinazotolewa,” alisema.