Arsenal Vs Liverpool: The Reds wana majeraha tele, nao ‘ndovu’ wakijaribu kurudi juu ya mti
UPDATE 21:30: Arsenal yashinda 3-1 ugani Emirates
NA LABAAN SHABAAN
KAMBI za klabu za Uingereza, Arsenal na Liverpool, zimezagaa ripoti za majeraha na wachezaji muhimu kuwa nje ya kipute cha kukata na shoka leo jioni.
Arsenal waliodumu juu ya msimamo wa ligi kuu ya kandanda Uingereza (EPL) kwa muda mrefu watashuka ugani Emirates kujaribu kukaribia kilele baada ya kudunguliwa na Liverpool – waliofungua mwanya wa alama 5.
Kiungo mkabaji wa Arsenal, Thomas Partey yuko mkekani kwa jeraha la paja naye mlinzi Takehiro Tomiyasu anawajibikia timu yake ya taifa la Japan.
Fabio Vieira na Jurrien Timber bado wanasubiri muda mrefu kidogo kurejea ugani.
Wenye hofu zaidi kwa kukosa wachezaji nyota ni Liverpool ambao wanatarajia kukosa huduma za mastaa Mohamed Salah, Darwin Nunez (huenda akacheza), Alex Mac Allister, Wataru Endo, Kostas Tsimikas na Stefan Bajcetic.
Arsenal watatoana jesho na Liverpool wakiwa na historia mbovu ya kutoshinda ikizingatiwa wameibuka washindi mara mbili katika mechi 17 zilizopita za ligi.
Vijana wa Mikel Arteta watatumia motisha ya uga wa Emirates kufufua moto wa ushindi wa nyumbani wa July 2020 na Oktoba 2022.
Msimu huu, Arsenal imecharaza timu saba za nje ya London zilizokaribishwa Emirates: takwimu mbaya kwa vijana wa Jurgen Klopp ambao watahitajika kukaba mawinga wa Arsenal wenye uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu.
Liverpool si wazuri kuzuia mawinga wenye kasi na stadi kama vile Gabriel Martinelli, Gabriel Jesus na Bukayo Saka ambao washiriki mchuano huu.
Wachambuzi wa kandanda wanasema hii ni mechi ambayo the Gunners hawafai kupoteza wakitaka kuweka hai matumaini ya kubeba kombe la EPL ambalo limewaepuka kwa miongo miwili.
“Lazima Arsenal ishinde. Wakipigwa wasahau kombe la EPL na hata sare haitawasaidia,” alisema Paul Merson, mchezaji wa zamani wa Uingereza ambayo anayeamini fomu nzuri ya Liverpool itakuwa kizungumkuti kwa Arsenal.
Endapo Arsenal itashinda, watafinya tofauti ya alama na Liverpool hadi pointi mbili.
Arsenal, Manchester City na Aston Villa wanafunga nne bora kwa alama sawa za 46, Liverpool wakiongoza kwa alama 51.