Afya na Jamii

Sababu zinazozima moto miongoni mwa wanawake chumbani

February 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA PAULINE ONGAJI

KUNA baadhi ya wanawake ambao hufika wakati wakakumbwa na tatizo la kukosa hamu ya mahaba, au kutofurahia tendo la ndoa.

Kumbuka kwamba furaha na msisimko wa tendo la ndoa hutegemea na masuala mengi ya kimwili hasa kwa wanawake.

Shida ya kukosa msisimko wa mahaba hutokea hasa baada ya mwanamke kujifungua. Wakati huu mtoto huwa na mahitaji mengi, kumaanisha kwamba mwanamke huwa amechoka sana wakati ambapo anapaswa kushiriki tendo la ndoa.

Pia, mwanamke akinyonyesha kuna homoni ambazo mwili huhitaji ili kuzalisha maziwa, ambapo pia zaweza kupunguza ashiki.

Mbali na hayo, kuna baadhi ya wanawake ambao hamu yao huathiriwa na hofu ya kushika mimba.

Aidha, matatizo katika uhusiano au ya kisaikolojia yanaweza kuchangia hali hii.

Wakati huu haifai mhusika kuhukumiwa, na badala yake, suala hili linapaswa kujadiliwa kwa uwazi.

Ili kuzuia hali hii, kama mwanamke unapaswa kuchukua muda kuomba usaidizi hasa kutokana na kazi za nyumbani ili upate wakati wa kupumzika.

Vilevile, litakuwa jambo la busara kuzungumza na mwenzio ili mjaribu mbinu za kuimarisha msisimko wa mahaba chumbani.