Magenge ya wizi wa mafuta mji wa Makutano, Mwea yaweka hatari ya mlipuko wakati wowote
Na MWANGI MUIRURI
WAKAZI wa mji wa Makutano ulioko katika mpaka wa Kaunti za Embu na Kirinyaga ukielekea Nyeri kutoka Kenol wanaishi katika hofu ya kukumbwa na mkasa wa mlipuko wa petroli.
Hii ni kufuatia harakati za wezi wa mafuta katika eneo hilo na ambapo wakishakamua mafuta hayo kutoka magari ya usafirishaji bidhaa za petroli, mizigo na abiria huishia kuhifadhiwa kiharamu katika maeneo ya makazi.
“Tumekuwa tukiteta kuhusu magenge haya kwa muda mrefu. Hatari ya milipuko kutukumba imekuwa ikituandama kwa polepole. Kwa sasa mji huu unazidi kupata idadi kubwa za watu wakihamia hapa. Tutalipuliwa,” akateta Bw Eudias Kaseve.
Bw Kaseve alisema kwamba “kwa siku moja hapa makutano huwa na zaidi ya lita 10,000 ambazo hukamuliwa katika kila aina ya ukora na kufichwa katika vyumba vya kimagendo”.
Taifa Leo Dijitali ilikumbana na magenge hayo ambayo hutekeleza ujambazi huo hadharani mchana na usiku.
Katika mtandao huo, malori yanayosafirisja bidhaa za mafuta hufyonzwa na madereva kulipwa.
Wengine ambao huuza mafuta yao kwa magenge hayo ni madereva wa malori, wale wa magari ya uchukuzi na wale wa magari ya kampuni na pia wa serikali.
Vijana hutokea kila kona ya mji wakibeba mitungi na mipira na baada ya kukamua, hukimbia na mitungi iliyojaa mafuta hadi kwa vibanda na manyumba ya kibinafsi kuyaficha.
“Cha kushangaza ni kwamba, baadhi ya ukora huo hutekelezwa machoni mwa polisi nje ya kituo cha askari wa Makutano huku pia kukiwa na ushirika wa kuokota hongo kutoka kwa wamiliki wa vibanda hivyo vya kuficha mali haramu,” akasema mwenyeji Bw Peter Ruku.
Aliyekuwa Naibu Kamishna wa Mwea Bi Jane Manene aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba hata yeye alishindwa kuelewa jinsi mtandao huo wa mafuta huepuka mkono wa sheria.
“Sisi tulikuwa tunapata habari za ujasusi na za tetesi kuhusu ukora huo. Hali hiyo ilikuwa inasemwa wa kuizima ni mamlaka ya uthibiti biashara ya nguvu za nishati na zile za mafuta (EPRA), ” akasema.
Alikiri kwamba ni ukweli kwamba mtandao huo uko na hutekeleza wizi wa mafuta hadharani.
Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi alisema kwamba “sakata hiyo ya wizi wa mafuta inatutatiza katika barabara ya Kenol hadi Makutano”.
Alisema kwamba mafuta hayo yanaathiri mazingira na pia kuhatarisha maisha ya watu.
“Hali hii ya hatari ni kupitia mafuta hayo ya wizi kuuzwa katika vituo vya mafuta eneo hili na pia kusafirishwa na kuhifadhiwa kupitia uchukuzi wa umma na ndani ya maeneo ya makazi,” akasema.
Bw Murungi alisema kwamba mafuta hayo huhatarisha usalama wa magari ambayo huishia kuyanunua huku nao wenye magari na makampuni ambayo hutekelezewa ukora huo wakienda hasara kuu.