Savula na wake zake wawili kuongezewa mashtaka mengine ya ufisadi
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Igonga atamwongezea Naibu Gavana wa Kaunti ya Kakamega Ayub Savula, wake wake wawili na washtakiwa wengine 12 mashtaka zaidi katika kesi ya kashfa ya kupora serikali Sh122 milioni miaka sita iliyopita.
Kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Henry Kinyanjui, DPP alifichua kwamba Bw Savula, wakewe Melody Gatwiri, Hellen Jepkor Kemboi na waliokuwa maafisa wakuu katika mamlaka ya kudhibiti matangazo ya serikali (GAA) wataongezewa mashtaka.
Kwa sasa wanakabiliwa na mashtaka 11 ya kula njama ya kuilaghai Serikali Sh122,335,500.
Savula, Melody na Hellen na kampuni zao saba za uchapishaji wameshtakiwa kupokea Sh122,335,500 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa serikali wakidai walikuwa na uwezo wa kuchapisha matangazo katika majarida yanayosambazwa mahala kwingi.
Bw Kinyanjui alisema hayo mbele ya hakimu mkuu wa Mahakama ya Milimani Lucas Onyina alipowaachilia rasmi washukiwa 13 waliokuwa wameshtakiwa pamoja Bw Savula.
Bw Onyina alitamatisha rasmi mashtaka dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Utangazaji, Bw Sammy Ishiundu Itemere na washtakiwa wengine 12.
“Kutokana na ombi la DPP, sina budi ila kuwaachilia washtakiwa 13 kwani hakuna ushahidi wa kuunga mkono kesi inayowakabili. Mmeachiliwa huru,” Bw Onyina aliamuru.
Wengine walioachiliwa ni Edith Kainda Nkanata, Amos Matanga Tayari, Gladys Hadida Bwora, Gladys Isaka Mwanyika, Agren Jesca Ateka, Rachel Wanjiru Munge, Nellie Kibocha Nyachomba, Sammy Makau Mule, Martin Njoroge Njenga, Hannah Wangari Wanderi, Edmund Horrace Munene na Victor Owino Achola.
Watakaoendelea na kesi ni Bw Savula, Melody, Hellen na kampuni zao saba ambazo ni Sunday Publishers Limited, Melsav Company Limited, Johnnewton Communications, The Express Media Group, No Burns Protection Agencies Limited, Cross Continents Ventures Limited na Shield Lock Limited.
Watumishi wa umma ambao hawakuondolewa kesi ni pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa kitengo cha utangazaji (GAA) Bw Dennis Kuko Chebitwey ,Dickson Onala Nyandiga, Fredrick Okello Owiti na Joseph Kamau Charagu.
Kuondolewa kwa mashtaka dhidi ya washtakiwa hao 13 kulifuatia utathmini upya wa ushahidi katika kashfa hiyo.
Wakati kesi hiyo imekuwa ikiendelea washtakiwa wawili Henry Mungasia Musambaga na Tabitha Nyaboke Oriba waliaga na kesi dhidi yao kutamatishwa.
“Baada ya kutathmini ushahidi uliopo dhidi ya washtakiwa 13 ni bayana hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kesi dhidi yao. Naomba mahakama ifitulie mbali kesi inayowakabili,” Bw Kinyanjui alimweleza Bw Onyina.
Wakili Ashitiva Mandale hakupinga ombi hilo dhidi ya washtakiwa hao 13 akisema “miaka sita imepita tangu washukiwa hawa wafikishwe kortini.Walipoteza kazi na mapato lakini hawapingi kesi dhidi yao ikizamishwa.”
Kesi hiyo itaendelea Aprili 21, 2024.