Je, unajua utaratibu wa kumuoa msichana wa Kikikuyu?
NA WANDERI KAMAU
MIONGONI mwa jamii za Kiafrika, ulipaji mahari ni miongoni mwa masuala muhimu yanayozingatiwa ili mwanamume aruhusiwe kumwoa msichana.
Ingawa mpenyo wa usasa umevuruga baadhi ya tamaduni zilizokuwa zikizingatiwa na jamii hizo, jamii ya Agikuyu bado inatilia maanani baadhi ya desturi zake, kwa ufano ulipaji mahari.
Majuzi, mwandishi huyu alihudhuria hafla ya ulipaji mahari katika eneo la Equator, Kaunti Ndogo ya Ndaragwa, Kaunti ya Nyandarua, na kujifunza mengi kuhusu taratibu za ulipaji mahari katika jamii hiyo.
Kabla ya mwanamume kuruhusiwa kufanya harusi, lazima akamilishe taratibu zote za ulipaji mahari.
Ikiwa msichana alitoroka kwao na kwenda kwa mwanamume bila kuwaambia jamaa zao, huwa hitaji la mwanamume huyo kuripoti kwamba alimchukua msichana wa wenyewe.
Maana halisi ya hatua hiyo huwa ni kuiambia familia ya msichana huyo kutomtafuta mwanao kwani yuko mahali salama.
“Mwanamume hujishtaki kwamba alichukua msichana huyo, hivyo hawafai kumtafuta mahali popote,” asema Mzee Geoffrey Mukundi, ambaye amekuwa akishiriki kwenye hafla hizo.
Anasema kuwa mwanamume anapoenda kujishtaki, huwa kuna ada fulani anayowalipa wazazi au walezi wa mwanamume huyo.
Hatua ya pili huitwa “mwati na harika” (kutoa kondoo au mbuzi). Katika hatua hii, mwanamume hutoa ada fulani ya kueleza nia ya kumwoa au msichana husika.
“Hapa, mwanamume huwa anaeleza nia ya kumwoa msichana huyo, hivyo hakuna mtu anayefaa kudai kumwoa. Hata hivyo, huwa anatoa ada fulani—kwa njia ya pesa (zinazohesabiwa kama mbuzi),” akaeleza Mzee Mukundi.
Pia, mwanamume huwa hatozwi pesa au “mbuzi” nyingi, kwani huwa ni hatua za mwanzo mwanzo za “kumnunua” msichana.
Hatua ya tatu huwa inaitwa ‘kumenya mucii’ (yaani kujua nyumbani kwa msichana aliyepangiwa kuozwa).
Katika hatua hii, mwanamume anayepanga kumwoa msichana huwa anatozwa ada fulani kama “kiingilio” cha nyumbani kwa msichana huyo.
“Hatua hii huwa ya kumruhusu mwanamume kujuana na jamaa za msichana anayepanga kumwoa, kama vile wazazi wake na jamaa zake,” asema Mzee Kamau Mundia.
Hatua ya nne huitwa ‘kuhaanda ithigi’ (au kupanda tawi). Kulingana na wazee, hapa ndipo mchakato halisi wa ulipaji mahari huwa unaanza.
Wanasema kuwa katika hatua hii, ndipo mwanamume huwa anatoa arbuni—yaani malipo ya kwanza ya ‘kumnunua’ msichana.
“Katika hatua hii, mazungumzo ya kina huwa yanaanza. Ni katika hatua hii ambapo wazee huwa wanashirikishwa ifaavyo. Ni katika hatua hii ambapo huwa wanaitisha pombe yao ya kienyeji. Akina mama pia huitisha malipo yao kwa mwanamume anayemwoa msichana. Kutokana na mabadiliko ya nyakati, malipo yote huwa yanatolewa kwa njia ya pesa, badala ya mbuzi, kama ilivyokuwa katika nyakati za hapo awali,” asema Mzee Mundia.
Hatua ya mwisho huwa ni ulipaji mahari wenyewe, yaani ‘ruraacio’ au ‘kuraacia’.
Katika hatua hii, familia ya msichana huwa inatoa usemi wake.
Huwa inaeleza bei ambayo ingetaka ‘kumuuza’ mwanao. Ni katika hatua hii ambapo pia wazee wanaomwakilisha mwanamume huwa wanazungumza na wale wa upande wa msichana ili kuafikiana kuhusu ni mbuzi wangapi (bei au gharama) ambayo mwanamume atamuuzia msichana.
Hapa, mwanamume huwanunulia wazee pombe yao (ya kienyeji), kwani ni wao pekee huwa wanaoshiriki katika hatua hiyo.
“Hii huwa ni hatua ya wazee pekee. Hivyo, mwanamume lazima awe amejitayarisha vilivyo kutimiza matakwa yao, kama shukrani kwa kumsaidia kupata msichana,” asema Bw Mundia.
Baada ya hatua hii, mwanamume huwa huru kumchukua msichana huyo kama mkewe, bila deni lolote.