Habari za Kitaifa

Jasho kupata kitambulisho, umepitia yapi kusaka stakabadhi hii?

February 6th, 2024 3 min read

Na WAANDISHI WETU

WAKENYA wanapitia mateso na kukaa kwa muda mrefu kabla ya kupata kitambulisho cha kitaifa ambacho ni haki yao ya kikatiba.

Inafaa kuchukua karibu mwezi mmoja kwa Mkenya aliyetuma ombi kupata kitambulisho cha kitaifa kukipata, kulingana na mwongozo wa utoaji wa huduma wa Halmashauri ya Kitaifa ya Usajili (NRB), inayotekeleza jukumu la kutoa stakabadhi za utambulisho kwa watu nchini.

Hata hivyo, hali ni tofauti kwa maelfu ya Wakenya ambao wamekuwa wakifika katika vituo vya kuchukua vitambulisho hivyo kila siku, kote nchini.

Kwa kawaida, ucheleweshaji huo umekuwa ukisababishwa na matatizo ya kimitambo, kama vile kuharibika kwa mashine za kuchapisha stakabadhi hizo, upungufu wa vifaa vya kuchapishia na hitaji kwa baadhi ya watu wanaotuma maombi kutoa maelezo ya kutosha ya utambulisho.

Mrundiko uliopo, hata hivyo, umesababishwa na agizo la mahakama kwamba serikali inafaa kusimamisha utoaji wa vitambulisho vya kidijitali.

Hali hiyo imesababisha mahangaiko kwa zaidi ya wanafunzi nusu milioni waliomaliza masomo yao ya shule za upili, hasa wanaotaka kuingia katika vyuo vikuu, watu wanaotafuta kazi, wagonjwa wanaotafuta paspoti ili kwenda ng’ambo kupata matibabu miongoni mwa Wakenya wengine.

Katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, watu waliotuma maombi ya kupata vitambulisho bado hawajapata.

Kitambulisho huwa stakabadhi muhimu, ambayo humwezesha mtu kupata huduma muhimu za serikali na sekta ya kibinafsi.

Wengi wanasema walituma maombi yao miezi kadhaa iliyopita, lakini hawajapata taarifa yoyote kuhusu ni lini watapokea stakabadhi hizo.

“Nimekuwa nikifika katika afisi ya usajili kwa miezi minne iliyopita, lakini nimekuwa nikiambiwa niendelee kufuatilia.

“Niliambiwa ucheleweshaji unatokana na hitilafu za kimitambo,” akasema Bi Rose Kemboi, mmoja wa watu waliotuma maombi ya kupata kitambulisho katika afisi ya usajili ya Uasin Gishu.

Maafisa wa usajili katika afisi ya Uasin Gishu wanakubali kuhusu uwepo wa ucheleweshaji wa utoaji wa stakabadhi hizo.

Wanahusisha hali hiyo na kesi ambayo imekuwa ikiendelea mahakamani.

“Agizo la mahakama kusimamisha utoaji wa vitambulisho vya kidijitali umevuruga mchakato mzima kwa kiasi kikubwa,” akasema afisa mmoja wa ngazi za juu wa usajili, ambaye hakutaka kutajwa.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia, kulikuwa na ongezeko la maombi ya watu kutaka vitambulisho mnamo Desemba.

Kwa wastani, maombi hayo yamekuwa kati ya 2,500 na 3,592.

Hata hivyo, Msajili wa Watu katika Kaunti, Bi Miriam Cheruwon, alihusisha ongezeko la maombi hayo na pendekezo la serikali kuongeza ada zinazotozwa ombi la kupewa vitambulisho vipya na kupata stakabadhi zilizopotea au zilizoharibika.

Bi Cheruwon anasema kuwa kuna vitambulisho vipya 1,070 katika idara ya usajili ambavyo havijachukuliwa na wenyewe, na nakala nyingine 1,800 ambazo hazijachukuliwa katika Kituo cha Huduma Centre.

Ikizingatiwa kuwa ni kaunti iliyo eneo la mpakani, Trans Nzoia huwa na hitaji la kuhakikisha kuwa watu wanaotuma maombi ya kupata vitambulisho si raia wa mataifa jirani.

“Huwa tunafanya upigaji msasa ambao wakati mwingine huchelewesha mchakato huo. Kufikia sasa, huwa tunatoa vitambulisho bila kuchelewa; kwa muda wa mwezi mmoja,” akasema Bi Cheruwon.

Katika Kaunti ya Turkana, kiongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Vyuo Anuwai na Vyuo Vikuu katika kaunti hiyo, Michael Ali, anasema kuwa serikali inafaa kutoa njia mbadala kwa wanafunzi kutuma maombi ya kupata mikopo, ufadhili wa masomo na basari bila vitambulisho.

Wanafunzi wengi waliomaliza sekondari katika kaunti hiyo wanaosubiri kujiunga na vyuo vikuu na vyuo anuwai, hawawezi kutuma maombi ya kupata mikopo kutoka kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) bila vitambulisho.

Wanafunzi wengine katika sehemu tofauti nchini wanakabiliwa na hali kama hizo.

Miongoni mwao ni barobaro Sam Nguru, aliye mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Pwani iliyo katika Kaunti ya Mombasa.

Kijana huyo anasomea uhandisi. Baada ya kutimu miaka 18, Desemba mwaka uliopita, ameanza kujawa na mashaka kuhusu kitambulisho cha kitaifa, kwani anakihitaji ili kutuma ombi la kupata mkopo wa HELB.

Pia, anahitaji kusajili kadi yake ya simu ili kuwasiliana na kumwezesha kutuma na kupokea pesa.

Hali ni kama hiyo katika kaunti kama vile Kisumu, Homa Bay, Marsabit miongoni mwa nyingine.