Makala

Chama cha wanaume chazua gumzo Meru

February 6th, 2024 2 min read

NA GITONGA MARETE

KWA miaka mingi, Wakenya wamezoea vyama vya wanawake vinavyoundwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Hii ndiyo sababu kikundi cha wanaume cha Kwa Njiru Men’s Welfare Self-Help eneo la Igembe ya Kati, Kaunti ya Meru kimeibua hisia miongoni mwa wakazi walioshtuka walipowaona wanaume wakikutana katika uwanja wa kanisa na kutangaza kuunda chama hicho.

Kwa zaidi ya miaka mitano, wanaume hao, wengi wao wakiwa na umri wa miaka 50 na 60, walikuwa wakikutana katika kituo cha biashara cha eneo hilo ili kujumuika na kucheza bao almaarufu Ajua, mchezo wa wazee kupitisha muda.

Walipokuwa wakicheza, walizungumzia matatizo yanayoikabili jamii na kuamua kuyapa ufumbuzi.

Kwa muda mrefu, eneo hilo limekuwa likikumbwa na changamoto nyingi zikiwemo unywaji wa pombe na dawa za kulevya, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, umaskini na dhuluma za majumbani.

Walikuwa na wasiwasi kwamba vijana wanazidi kupotelea katika pombe za kienyeji, jambo ambalo lilitishia kizazi kizima.

Ajira ya watoto katika mashamba ya miraa pia imekithiri, hali walioapa kuikomesha, hata waliposhughulikia suala tata la kukodisha mashamba ya miraa.

Stephen Kaberia, mwenyekiti wa kikundi hicho anaeleza kuwa mwaka jana, aliibua wazo la kutatua changamoto hizo. Anasema wanawake waliposikia wanaume walikuwa wakikusanyika kwa nia ya kuanzisha chama, waliwacheka.

“Watu walidai kuwa tunakutana kupanga mikakati ya jinsi ya kuwainua wanawake, wakisema mipango yetu ilikuwa mibaya. Hii ilikuwa kwa sababu pia hatuwaruhusu wanawake miongoni mwetu,” Kaberia alisema katika mahojiano katika maskani’ yao katika steji ya Kwa Njiru, Wadi ya Athiru Gaiti.

Baada ya kusajili kikundi hicho Machi mwaka jana, walianza kuweka akiba ya Sh200 kila wiki kila mwanachama na hadi mwisho wa mwaka huo walikuwa na Sh800,000 kwenye akaunti yao.

Pia wana kanuni za kushangaza. Wanachama hawaruhusiwi kuhudhuria mikutano wakiwa wamelewa. Pia ni marufuku kwa mwanachama kuvuta bangi.

Huwa wanashirikiana na machifu na wanachama wa mpango wa Nyumba Kumi katika kutekeleza kanuni hizo. Faini ya Sh500 hutozwa kwa yeyote anayekiuka sheria na huwa katika hatari ya kufukuzwa chamani.

Kwa sasa kina wanachama 120 na bado kinaimarika huku vijana wakijiunga nao.

“Wanajamii wametambua na kuthamini jukumu lao wakisema ni kubwa kuliko lile la kikundi cha wanawake,” Kaberia anasema.

“Tulitaka kutoa ujumbe kwa hivyo mnamo Desemba 20, 2022, tulitoa fedha na kugawana kulingana na akiba ya kila mwanachama.

Baadhi yetu tulienda nyumbani na Sh100,000. Tuliandaa karamu ya wanaume na ilikuwa ya kusisimua. Wanachama wetu walinunulia wake wao zawadi za Krismasi na kulipa karo ya shule ya watoto wao.