Makala

Wakazi wa Lamu waliozoea mikweche sasa waletewa mabasi manyanga

February 8th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Kaunti ya Lamu ambao miaka kadhaa iliyopita walizoea magari mikweche, sasa ni wenye furaha tele kwani wamiliki wengi wa magari ya usafiri wa umma eneo hilo wamewaletea mabasi mapya almaarufu manyanga katika miaka ya hivi karibuni.

Zamani kabla ya barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen kujengwa na kukamilika, kampuni nyingi za magari ya usafiri wa umma zilipendelea kupeleka mabasi mzee kuhudumia wasafiri wa Lamu kutokana na ubovu uliokithiri kwenye barabara hiyo.

Aghalabu wasafiri walikuwa wakiishia kuchelewa kufika kwani magari hayo makuukuu mara nyingine yaliishia kuchomoka vipuri njiani au katikati ya safari, hali iliyoaminika kuchangiwa na ubovu wa barabara.

Barabara ya Lamu-Witu-Garsen, ambayo ni ya kilomita 135, ilijengwa na kukamilika hadi kufunguliwa rasmi na Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta mnamo Mei 20,2021.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo kati ya 2021 na 2024 umebaini kuwepo kwa magari mengi mapya–manyanga–ya usafiri wa umma yanayohudumu kwenye barabara hiyo, hali ambayo imeleta afueni na furaha riboribo kwa wasafiri.

Bi Amina Abdulkarim, mkazi wa Mokowe, anasema ni raha kwamba angalau wakazi wa Lamu nao wanaweza kujichagulia gari la kusafiria kinyume na awali ambapo magari yenyewe yalikuwa makuukuu na machache ajabu.

“Twashukuru kuletewa mabasi, matatu na hata probox mpya mpya za kusafiria kwenye barabara yetu ya Lamu-Witu-Garsen. Zamani magari ya usafiri wa umma yalikuwa machache na yenye kuzeeka kwelikweli. Ni ajabu kwamba leo hii msafiri wa Lamu naye anaweza kuchagua ni gari gani la kusafiria. Je, ni jipya au mzee? Twajihisi kama wakenya wengine sasa,” akasema Bi Abdulkarim.

Mohamed Yusuf, mkazi wa kisiwa cha Lamu, anasema msafiri wa Lamu angalau amepunguziwa presha za kukimbilia gari ambayo wakati huo zilikuwa moja au mbili na zilizosafiri wakati fulani pekee, iwe ni asubuhi mapema au jioni ya kuchelewa.

“Kuvuka kutoka kisiwani Lamu hadi jeti ya Mokowe ili upande gari tayari ni tatizo. Wakati huo magari yalipokuwa machache ulilazimika kuamka asubuhi ili kuwahi gari. Ulikuwa ukikosa gari husika unalazimika kusafiri usiku au siku iliyofuata. Twashukuru kwani leo hii magari ni mengi na mapya. Twajipanga wenyewe ni jinsi gani tutasafiri. Hamna tena presha,” akasema Bw Yusuf.

Bi Leila Athman hakuficha furaha yake kufuatia wamiliki wengi wa magari ya usafiri wa umma kuweka mabasi au matatu manyanga kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Basi jipya na la kisasa linalohudumia wasafiri kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Athman anasema inavyoonekana ni kama kuna ushindani mkali wa kibiashara kati ya wamiliki wa mabasi ya usafiri wa umma wanaohudumia abiria kwenye barabara ya Lamu-Witu-Garsen kwani kila mmoja sasa anang’an’ania kuweka gari jipya barabarani ili kuvutia wateja.

“Ushindani wa wamiliki wa magari ya usafiri wa umma kimuonekano wa magari yao ni baraka kwetu. Angalau tunasafiri raha mustarehe kwenye magari mapya. Hili pia limesaidia kuharakisha safari zetu. Magari makuukuu yaliharibikia njiani kila mara. Hali ya sasa ni shwari,” akasema Bi Athman.

Baadhi ya wamiliki wa magari ya usafiri wa umma waliohojiwa na Taifa Leo walikiri kushindana katika kuhakikisha magari wanayoweka kuhudumia wasafiri barabarani ni yenye mvuto na shwari.

Basi jipya na la kisasa linalohudumia wasafiri kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Ahmed Swaleh, anasema endapo mmiliki wa magari ya usafiri wa umma atapuuzilia mbali hali au muonekano wa gari lake, basi atajilaumu mwenyewe.

“Ukichelewachelewa utampata mwana si wako. Inabidi tujikaze kuweka magari mapya barabarani na ambayo yako katika hali nzuri. Usipofanya hivyo utapoteza wateja kwa mwenzako ambaye magari yake ni mapya na ya kuvutia. Tunajikaza ili kudumu biasharani,” akasema Bw Swaleh.

Serikali kuu ilijenga barabara ya Lamu-Witu-Garsen kwa kima cha Sh10.8 bilioni.

Kukamilika kwa barabara hiyo pia kumesaidia pakubwa kuleta mfumko wa kibiashara na kupanuka kwa kaunti ya Lamu na eneo la Kaskazini mwa Kenya kwa jumla.