Mzigo wa kansa waendelea kulemea wengi duniani
NA PAULINE ONGAJI
MZIGO wa maradhi ya kansa uneandelea kuongezeka.
Haya ni kulingana na makadirio yaliyotolewa na Shirika la kimataifa linalohusika na utafiti wa maradhi ya kansa (IARC).
Aidha, Shirika la Afya Duniani limechapisha matokeo ya aua kutoka mataifa 115, inayoonyesha kwamba nchi nyingi hazipi matibabu ya kansa kipaumbele, kama sehemu ya huduma ya afya kwa wote (UHC).
Aua ya WHO kuhusu UHC na kansa inaonyesha kwamba ni asilimia 39 pekee ya mataifa yaliyoshiriki, ambayo yalihusisha tiba ya kansa kama mojawapo ya huduma zinazogharimiwa.
Aidha, ni asilimia 28 pekee ya nchi zilizoshiriki ziligharamia huduma zingine za matibabu ya kansa, kama vile huduma ya kukabiliana na makali ya dalili za maradhi haya.
Kulingana na makadirio ya IARC, katika mwaka wa 2022 kulikuwa na takriban visa milioni 20 vipya vya kansa na vifo milioni 9.7. Idadi ya wagonjwa ambao waliendelea kuishi kwa miaka mitano baada ya kugundulika kuugua maradhi haya, ilikuwa milioni 53.5. Takriban mmoja kati ya watu watano hukumbwa na kansa, na takriban mmoja kati ya wanaume tisa na mmoja kati ya wanawake 12, hufariki kutokana na ugonjwa huu.
Kulingana na makadirio haya mapya ya IARC, aina 10 za kansa ziliwakilisha theluthi mbili ya visa vipya na vifo mwaka wa 2022.
Kansa ya mapafu ndio aina ya kansa iliyoonekana kukithiri sana ulimwenguni, huku visa milioni 2.5 vipya vikiwakilisha asilimia 12.4 ya visa vyote vya maradhi haya, vipya vilivyonakiliwa.
Kansa ya matiti miongoni mwa wanawake iliorodheshwa ya pili (visa milioni 2.3, asilimia 11.6), ikifuatiwa na kansa ya utumbo (visa milioni 1.9, asilimia 9.6), kansa ya tezi ya uzazi (visa milioni 1.5. asilimia 7.3) na kansa ya tumbo (visa 970,000, asilimia 4.9).
Aidha, kansa ya mapafu ndio inayoongoza kwa kusababisha vifo (vifo milioni 1.8, asilimia 18.7 ya jumla ya idadi ya vifo), ikifuatiwa na kansa ya utumbo (vifo 900,000, asilimia 9.3), kansa ya ini (vifo 760 000, asilimia 7.8), kansa ya matiti (vifo 670 000, asilimia 6.9) na kansa ya tumbo (vifo 600 000, asilimia 6.8).
Inatabiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2050, kutakuwa na visa milioni 35 vipya vya kansa, idadi ambayo ni ongezeko la asilimia 77 kutoka kwa visa milioni 22 vilivyokadiriwa mwaka wa 2022.
Mzigo huu wa kansa unatokana na masuala tofauti kama vile idadi kubwa ya watu walio na umri mkubwa, mabadiliko ya mitindo ya maisha, vilevile, idadi kubwa ya watu wanaoendelea kuwa wazi kwa vihatarishi vinavyosababisha kansa kama vile tumbaku na hewa chafu.