Mbali na Kiptum, fahamu wanariadha wengine kutoka Kenya waliohusika katika ajali mbaya
Na GEOFFREY ANENE
KIFO cha mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 42 Kelvin Kiptum kinaibua maswali mengi, hasa kwa sababu yeye siye mwanariadha wa kwanza Mkenya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani.
Nicholas Bett alifariki miezi michache baada ya kuibuka bingwa wa dunia wa mbio za mita 400 kuruka viunzi mwaka 2015.
Orodha ya wanariadha waliohusika katika ajali za barabarani ni ndefu.
Kipchoge, mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za mita 800 David Rudisha, gunge wa marathon, mbio za nyika na 21km Geoffrey Kamworor, bingwa wa dunia wa kurusha mkuki mwaka 2015 Julius Yego na bingwa wa zamani wa dunia wa 1,500m Asbel Kiprop pia waliwahi kuhusika katika ajali mbaya, lakini wakaponea kifo.
Rudisha alipata ajali katika barabara ya Keroka-Sotik miaka minne iliyopita. Gari lake la Landcruiser V8 liligongana na basi la kampuni ya EasyCoach. Rudisha aliponea kifo tena Desemba 2022 baada ya kuhusika katika ajali ya ndege katika eneo la Imbirikana katika kaunti ya Kajiado.
Mwaka 2010, bingwa wa zamani wa dunia mbio za mita 10,000 Moses Tanui alijeruhiwa vibaya mguu na kifua katika ajali ya barabarani. Alikuwa katika gari moja na mwanariadha David Lelei aliyefariki katika ajali hiyo iliyofanyika katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.
Ni mwaka 2010 pia wakati mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia ya marathon Paul Tergat alihusika katika ajali mbaya ya barabarani alipogonga lori katika eneo la Burnt Forest na kuhitaji matibabu katika hospitali ya Aga Khan. Tergat sasa ni rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K).
Mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia Wilson Kipsang alihusika katika ajali ya barabarani mjini Eldoret mwaka 2020 na tena Kolol katika kaunti ya Elgeyo Marakwet mwezi Januari 2023 akiponea kifo.
Bingwa wa Olimpiki mbio za mita 800 mwaka 2008 Wilfred Bungei aliponea kifo Septemba 2023 alipohusika katika ajali karibu na Chuo Kikuu cha Kabarak. Hiyo ilikuwa ajali ya pili ya Bungei baada ya kuponea kifo mnamo Mei mwaka 2012 akipaisha gari akiwa amelewa.
Mwezi Februari 2009, Jefferson Siekei alifariki akiwa na umri wa miaka 25 akiendesha pikipiki. Siekei aliyekuwa amerejea nyumbani kutoka Japan alikokuwa akiishi, aligongana ana kwa ana na lori.
Bingwa wa zamani wa Boston Marathon, Lameck Aguta alipata ajali katika kaunti ya Nakuru mnamo Julai 1997 na kuwa katika koma kwa miezi mitatu kabla ya kurejea mashindanoni.