Makala

Wanariadha wachanga waliofariki nyota zao zikiwa ndio zimeanza kung’aa

February 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

KIFO cha mshikilizi wa rekodi ya dunia  ya mbio za marathon, Kelvin Kiptum, Jumapili usiku, kimeibua kumbukumbu ya wanariadha waliofariki wakiwa wachanga, wakati nyota zao zilikuwa zinaanza kung’aa.

Kiptum, 24, alifariki kwenye ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Kaptagat, Elgeyo Marakwet. Alikuwa pamoja na kocha wake, Garvais Hakizimana ambaye ni raia wa Rwanda.

Mwanariadha huyo mahiri si wa kwanza kukumbana na mauti akiwa mchanga, wakati alikuwa ashaanza kujizolea umaarufu.

Baadhi ya wanariadha wengine waliofariki wakati walikuwa wameanza kuwika ni Samuel Wanjiru, Agnes Tirop, Nicholas Bett, Hosea Macharinyang’, David Lelei, Jefferson Siekei, Francis Kiplagat, Richard Chelimo kati ya wengine wengi.

Mwanariadha Samuel Wanjiru alikuwa ndiye bingwa wa mbio za wanaume za marathon katika mashindano ya Olimpiki, jijini Beijing, China, mnamo 2008.

Alikuwa ameshinda mbio nyingine kadhaa za marathon. Alifariki 2011 kutokana na majeraha aliyopata baada ya kile polisi walitaja kama kuanguka kutoka orofa ya nyumba yake mjini Nyahururu, Kaunti ya Nyandarua. Alifariki akiwa na umri wa miaka 24 pekee.

Anatajwa kuwa miongoni mwa wanariadha mahiri sana katika kizazi chake. Ndiye alikuwa Mkenya wa kwanza kushinda mbio za marathon za wanaume kwenye mashindano ya Olimpiki.

Mnamo Oktoba 2021, mwanariadha Agnes Tirop aliibukia bingwa mchanga sana wa mbio za masafa marefu za wanawake. Alikuwa na umri wa miaka 25 pekee alipofariki katika hali tatanishi mwaka uo huo.

Mwanariadha huyo mchanga alipatikana akiwa amefariki nyumbani kwake, mjini Iten, katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Tirop alishinda nishani ya shaba kwenye Mbio za Mashindano ya Dunia mnamo 2017 na 2019. Alimaliza wa nne kwenye mbio za mita 5,000 kwenye mashidano ya Olimpiki ya Tokyo mnamo 2020. Pia,  alivunja rekodi ya dunia kwenye mbio za wanawake za kilomita kumi.

Kufikia kifo chake mnamo Oktoba 2021, Hosea Macharinyang’ alikuwa miongoni mwa wanariadha ambao nyota zao zilikuwa zimeng’aa kweli kweli.

Alikuwa ameiongoza timu ya Kenya kushinda mara tatu kwenye Mashindano ya Dunia ya Mbio za Masafa Marefu kati ya 2006 na 2008.

Alipatikana akiwa amefariki nyumbani kwake katika eneo la Murkwijit, Kaunti ya Pokot Magharibi. Alikuwa na umri wa miaka 35.

Ripoti zilieleza alijitoa uhai wake.

Mwanariadha Gilbert Kwemoi alifariki mnamo Oktoba 2021, akiwa bado mchanga. Alikuwa na umri wa miaka 29.

Marehemu alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kulingana na familia yake, mwanariadha huyo alilalamikia maumivu ya kichwa, japo akafariki muda mfupi baaa ya kukimbizwa hospitali.

Alishinda medali ya dhahabu kwenye mbio za mita 1,500 kwenye Mashindano ya Olimpiki ya Vijana yaliyofanyika 2014, Nanjing, China.

Mapema mwaka huo, alikuwa ameshinda dhababu Mashindano ya Riadha ya Vijana Afrika jijini Gaborone, Botswana.