Mwadime awatetea mawaziri wanaoshinikizwa kujiuzulu kwa kuzembea
NA LUCY MKANYIKA
GAVANA wa Kaunti ya Taita Taveta Andrew Mwadime amewapuuza wakosoaji wake wanaomlaumu kwa kushindwa kuboresha sekta ya afya katika kaunti hiyo, akisema anahitaji muda zaidi na rasilimali ili atimize ahadi zake.
Gavana Mwadime alikuwa akizungumza katika eneo la Taveta wakati wa kuzindua ujenzi wa kiwanda cha kukoboa na kusafisha mpunga cha Sh45 milioni.
Gavana huyo alisema uhaba wa dawa na mashine za vituo vya afya vya kaunti hiyo sio kosa lake, bali umesababishwa na kucheleweshwa kwa fedha kutoka katika Hazina ya Kitaifa.
Alisema kaunti hiyo haijapokea mgao wake wa Desemba na Januari, hali ambayo imeathiri ununuzi wa dawa na mahitaji muhimu na vilevile malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa kaunti.
“Hatujazembea bali tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanapata huduma bora za afya. Lakini hatuwezi kufanya hivyo bila pesa. Ikiwa serikali kuu itatupatia fedha zetu kwa wakati unaofaa, tutaweza kukabiliana na changamoto zinazoikumba sekta yetu ya afya,” alisema.
Alisema utawala wake kupitia Idara ya Afya umetenga Sh20 milioni kila mwezi kwa ajili ya ununuzi wa dawa na bidhaa za matibabu kwa vituo vya afya vya kaunti hiyo.
Alisema kaunti hiyo imefanya mipango na Shirika la Usambazaji wa Dawa Nchini (Kemsa) na Shirika la Dawa za Dharura na Vifaa (Meds) ili kusambaza dawa kwa vituo vya afya kwa minajili ya kuwapa wananchi afueni kutokana na kununua dawa kutoka kwa maduka ya wamiliki wa kibinafsi.
“Kwa miezi miwili hatujapokea fedha zetu kutoka kwa serikali kuu na ndio maana tuna tatizo hili. Tunajua kuna matatizo yanayokabili idara hii lakini tunajitahidi kuyatatua,” alisema.
Kauli yake inajiri huku baadhi ya wakazi wakitaka kung’atuliwa ama kujiuzulu kwa Waziri wa Afya wa Kaunti ya Taita Taveta Gifton Mkaya kwa madai ya kutoa huduma duni katika vituo vya afya vya kaunti.
Waziri huyo pia amelaumiwa kwa kukubali uzembe katika vituo vya afya na hivyo kusababisha vifo na maafa makubwa kwa wagonjwa wanaotafuta huduma humo.
Gavana alisema hatamfuta kazi Bw Mkaya kwani maafisa waliohusika na matukio hayo walichukuliwa hatua kali za kinidhamu.
“Maafisa wa afya waliotuhumiwa na visa hivyo wamesimamishwa kazi. Hiyo inamaanisha tumechukua hatua kukabiliana na maswala ya utepetevu,” alisema.
Alisema mawaziri wake ni wachapakazi na wamejitolea kutekeleza maono yake ya kuleta maendeleo katika kaunti hiyo.
“Mawaziri wangu wote wa kaunti wametia saini mikataba ya utendakazi kwa hivyo tuwape muda wafanye kazi ili tuone mafanikio yao,” alisema.
Bw Mwadime pia alisema mawaziri wanafanya kazi kuhakikisha kuwa wanapata wafadhili wa kusaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika kaunti akisema fedha kutoka hazina ya kitaifa ni chache mno kufanya miradi mikubwa.
Alisema baadhi ya miradi iliyokwama wakati wa utawala uliopita itakamilishwa ili kuokoa fedha za umma.
Alifichua kuwa ujenzi wa kiwanda cha ndizi cha Sh110 milioni utarejea hivi karibuni.
Mradi huo ambao ulikuwa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na serikali ya kaunti ulikwama mwaka wa 2020 kutokana na madai ya ufisadi na kushindwa kwa utawala uliokuwa mamalakani kutimiza wajibu wake wa kufadhili.
“Tumepata mfadhili mwingine atakayekuja mwezi ujao. Kiwanda hicho kitaboresha mazao ya ndizi, muhogo, viazi vitamu na nduma,” alisema.
Pia aliwahimiza wakazi kuunga mkono serikali yake na kukataa kuhusishwa na siasa za mgawanyiko.
“Siogopi ukosoaji lakini usiwe na nia mbaya. Ukosoaji ni mzuri lakini naomba tuungane na viongozi wote ili tuendeleze kaunti yetu,” alisema.
Kiwanda hicho cha mpunga kinatarajiwa kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani ya mpunga katika kaunti hiyo.
Idara ya Kilimo inajitahidi kuhakikisha kuwa mmea wa mpunga ni moja ya mazao makuu yanayolimwa katika eneo la Taveta.
Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuboresha zaidi ya tani 72 za mpunga kwa siku na kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na vilevile kutoa nafasi za ajira kwa wenyeji wa eneo hilo.
Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Taita Taveta Eric Kyongo alisema kiwanda hicho kitakamilika kabla ya Juni 2024.
Alisema kiwanda hicho kitasimamiwa na Shirika la Maendeleo la Taita Taveta ambalo litahakikisha kuwa linanunua mazao yote kutoka kwa wakulima.
“Wakulima hawatakuwa na mzigo wa kuleta mazao kutoka mashambani hadi kuwandani. Kampuni hiyo ndiyo itakuwa na jukumu la kusafirisha mazao kutoka shambani hadi kiwandani,” akasema Bw Kyongo.