Men’s Conference: Kongamano la mashambulizi shtukizi ya kulinda ‘boychild’
NA WANDERI KAMAU
MIAKA michache iliyopita, neno ‘Men’s Conference’, yaani Kongamano la Wanaume, lilikuwa tamko tu la kimzaha kwenye mitandao ya kijamii wakati wa msimu wa Valentino.
Lilikuwa kongamano la kubuniwa, ambapo wanaume walikutana mitandaoni kujadili masuala yao, ili “kutosumbuliwa” na wanawake wao katika msimu huo wa Siku ya Wapendanao.
Watu walijaza ucheshi kwenye mitandao ya kijamii, kuhusu masuala ambayo yalijadiliwa kwenye kikao hicho.
Miongoni mwa misukumo mikuu ya kuandaliwa kwa kongamano hilo ni “kuwaepushia wanaume gharama zinazotokana na sherehe za siku hiyo.”
Mdahalo huo ulionekana kuwaunganisha sana wanaume katika mitandao hiyo, kiasi kwamba “wanachama” walimteua mwanasiasa na mfanyabiashara tajiri (marehemu) Jackson Kibor kutoka Kaunti ya Uasin Gishu kuwa “mwenyekiti”wa kongamano hilo.
Mjadala huo ulipoendelea kushika kasi, baadhi ya watu waliona ikiwa heri kuanza kukutana kihalisia, badala ya ucheshi huo kuishia tu kwenye mitandao ya kijamii baada ya siku hiyo kupita.
Kongamano hilo lilifanyika kwa mara ya kwanza mjini Eldoret mnamo 2019, ambapo Bw Kibor ndiye aliyekuwa mgeni wa heshima.
Kama lilivyoitwa, ni wanaume pekee walioruhusiwa kuhudhuria kongamano hilo.
Suala kuu lililoibuka kwenye kongamano hilo ni hitaji la jamii kuanza kumtetea na kumlinda mtoto wa kiume.
“Tunapowatetea wanaume kutambuliwa na jamii, ni jukumu lao kuwajibikia vitendo vyao. Nawashauri muwe waangalifu mnapowachagua wanawake, kwani kunao wazuri na wengine wasiojali maslahi ya mwanamume,” akasema Mzee Kibor.
Washiriki wengine wa kongamano hilo walikuwa ni Askofu Jackson Kosgei, aliyekuwa miongoni mwa waalikwa wakuu.
“Tunayopitia kwa sasa ni mgogoro wa utambulisho wa kijinsia. Mtoto wa kiume anapoteza nafasi na usemi wake katika jamii. Huu ni wakati wa kumrejesha ushawishi wake,” akasema askofu huyo.
Hali si tofauti mwaka huu, kwani kuna makongamano kadhaa ambayo yamepangiwa kufanyika, waandalizi wakisema kuwa lengo lao ni kutetea maslahi ya mwamamume katika jamii.
Waandalizi wa makongamano hayo ni Mhubiri Robert Burale na mwanahabari Stephen Letoo, ambaye ni ripota katika runinga ya Citizen.
Kongamano aliloongoza Bw Burale lilifanyika Jumamosi wiki iliyopita, ambapo ujumbe mkuu ulikuwa ni “kurejesha nafasi ya mwanamume katika jamii”.
Bw Letoo naye anashikilia kuwa lengo la kongamano lao (litakalofanyika kuanzia leo, Jumatano, hadi Jumapili) ni kuwapa nafasi wanaume “nafasi ya kukutana na kujadili changamoto zinazowakabili katika jamii”.
Ingawa kongamano hilo limekuwa likichukuliwa kimzaha na wengi, anasema kuwa lengo lao ni kuanzisha vuguvugu lenye nguvu, litakaloanza harakati za kuwatetea wanaume.
“Hili si suala la kimzaha. Ni mwanzo tu wa vuguvugu kubwa litalokuwa sauti ya wanaume waliotengwa na jamii. Ili kuonyesha uzito wa mkakati huu, tuna hadi afisi, ambapo wanaume wanaweza kutufikia na kuripoti changamoto wanazopitia,” akasema.